Harufu ya rushwa! Safu ya ulinzi katika
maduka ya biashara ya Mlimani City, Dar kwenye geti la kuingilia na lile
la kutokea, inadaiwa kutawaliwa na rushwa ambapo walinzi wamenaswa
‘laivu’ wakipokea ‘mlungula’.
Kwa mujibu wa walalamikaji, walinzi hao
wanadaiwa kujiwekea utaratibu usiyo rasmi chini ya kampuni ya ulinzi wa
eneo hilo iliyotajwa kwa jina la Omega Nitro Risk Solutions ya jijini
Dar ambapo ‘vijana’ wake wanatuhumiwa kutoza watu faini ya shilingi elfu
kumi kwa gari ambalo mhusika wake amepoteza kadi ya kuingia na kutoka.
Madai hayo yalikwenda mbele zaidi
ikielezwa kuwa kumekuwa hakuna utaratibu mahususi kwenye ishu hiyo kwani
baadhi ya walinzi kila mmoja hujiamulia kuchukua fedha bila mhusika
kupewa risiti ya malipo.
“Kuna tatizo kwenye safu ya ulinzi, huwa tunatozwa faini shilingi elfu kumi ukipoteza kadi,” alisema mmoja wa walalamikaji hao.
Baada ya malalamiko kutua kwenye kitengo
chetu cha Oparesheni Fichua Maovu (OFM), kazi ilianza ambapo kikosi
kazi kilifanya doria kwa siku kadhaa na kufanikiwa kunasa laivu hatua
kwa hatua, tukio la walinzi hao wakilamba ‘kitu kidogo’.
Tukio hilo lilijiri hivi karibuni katika
geti la Mlimani City la upande wa Barabara ya Sam Nujoma ambapo walinzi
hao walizuia gari la jamaa aliyekuwa amepoteza kadi na kuchukua rushwa.
Katika hali ya kushangaza au njaa,
tofauti na kiasi cha shilingi elfu kumi kilichotajwa awali, walinzi hao
walikubali kumpunguzia jamaa huyo hadi elfu tano bila kujua kwamba
walikuwa wakirekodiwa hatua kwa hatua.
Baada ya kujikusanyia ushahidi wa
kutosha, OFM ilizungumza na bosi wao ambaye ni Senior Inspector wa Omega
Nitro Risk Solutions, Leo John Masuka juu ya vitendo hivyo ambapo mbali
na kuonesha kushangazwa na habari hizo, pia alianika kila kitu jinsi
wanavyofanya kazi.
“Nashangaa kama kuna tatizo kama hilo
kwani tumesitisha kuwatoza faini wanaopoteza kadi, nitafanya uchunguzi
ili kuwabaini watu hao ambao wanaharibu sura ya kampuni.
Katika hali hiyo kwa kipindi hiki cha
tishio la ugaidi ni rahisi kwa magaidi kutoa rushwa kisha kuingia na
kufanya utekaji kama walivyofanya nchini Kenya kwenye maduka ya
Westgate.