Waraka wenye vitisho ukiwa na nembo ya Jumuiya ya Uamsho na mihadhara ya Kiislam (JUMIKI) umesambazwa visiwani Zanzibar, ukidaiwa kutishia kufanyika kwa shambulio dhidi ya viongozi wa dini na Serikali kabla ya Sikukuu ya Eid El Haj.
Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkadam Khamis Mkadam
amethibitisha kupata nakala ya waraka huo wenye maneno makali na vitisho
kwa usalama wa watu na amani ya nchi. Kamanda Mkadam alisema,Polisi imefanikiwa kuupata waraka huo baada ya tukio hilo kuripotiwa na baadhi ya viongozi wa madhehebu ya dini Visiwani humo.
Hata
hivyo, alisema,tayari makachero wa Polisi wako kazini na ametoa wito
kwa viongozi wa dini na wananchi kuondoa hofu kwa vile vyombo hivyo vya
ulinzi na usalama vimejiandaa kukabiliana na tukio lolote la kihalifu.
Aliwasihi wananchi kuendelea na jitihada za kuwafichua wahalifu na watu wanaowatilia shaka dhidi ya amani visiwani hapa.
“Hatua
tulizochukua ni pamoja na kuwataka viongozi wa dini kuanzisha kamati za
ulinzi mbali na kuwapatia huduma za ulinzi kama njia ya kukabiliana na
matukio mbalimbali,”alisema Kamanda Mkadam.
Waraka
huo unadaiwa kuainisha vitendo vya hujuma kuwa vitazidi hadi pale
Zanzibar itakapofanikiwa kurejesha kile kilichoitwa Uhuru wake.Source:Gazeti la Mwananchi