Serengeti. Juliana Marwa (14)mkazi wa Kijiji
cha Nyamakendo wilayani hapa mkoani Mara anadaiwa kujinyonga hadi kufa
kwa kutumia kamba ya katani kwa madai ya kumuhofia baba yake mzazi
kumlisha nyama mbichi.
Tukio hilo linasemekana kutokea baada ya marehemu
huyo kumpiga ndama na baada ya baba yake kumkuta alimtishia kumlisha
nyama mbichi ya ndama huyo iwapo atakufa kwa kipigo hicho.
Hata hivyo, tukio hilo limeacha maswali mengi kwa
wakazi wa kijiji hicho licha ya kuthibitishwa na diwani wa kata hiyo,
Samweli Gibewa na polisi wilayani hapa .
Akizungumza diwani huyo amesema, siku ya tukio,
saa 12 jioni msichana huyo akiwa anakamua maziwa ya ndama alikuwa
anamsumbua kwa kutaka kunyonya ndipo akaanza kumpiga, kitendo
kilichomuudhi baba yake na kumtolea maneno kuwa akifa atamla mbichi,
kauli inayodaiwa kumuudhi na kuamua kwenda kujinyonga.
“Alikutwa ndani ya shamba la mihogo mita 100
kutoka nyumbani kwao asubuhi kesho yake kwa kuwa baada ya kugombezwa
alitoweka kwao…mama yake alipokwenda shambani kupalilia ndipo akamkuta
ananing’inia na kulazimika kupiga kelele kuomba msaada,” alisema diwani.
Mama mzazi wa marehemu, Mugosi Marwa akielezea
tukio hilo alidai baada ya binti huyo kutoelewana na baba yake alitoweka
nyumbani usiku na kudhani ameenda kulala kwa bibi yake anayeishi jirani
hivyo hawakuwa na hofu wakijua atarudi asubuhi kinyume chake akaenda
kujinyonga.
Marehemu hakuacha ujumbe wowote juu ya uamuzi wake
huo huku Polisi wakidai kuendelea na uchunguzi kuhusiana na tukio hilo
baada ya kuhoji familia akiwamo baba mzazi Marwa Mwita Yahara.