Tuhuma ya mastaa Bongo kujihusisha na mambo ya ulozi au uchawi
imeibuliwa upya na safari hii bundi kajikita zaidi kwenye kiwanda cha
sinema za Kibongo, Ijumaa lina ripoti kamili.
UCHUNGUZI
Uchunguzi wa gazeti hili ndani ya
ulimwengu wa mastaa hao ulibaini kwamba, ukiwaacha wale wa Bongo Fleva
ambao wamekuwa wakishikana uchawi kila kukicha, kwenye filamu ndiko
hakufai.
Ilibumburuka kwamba masuala ya kurogana ndiyo yamesababisha filamu za baadhi yao kudoda na kukosa soko.
Inaelezwa kwamba mbali na sinema zao kubuma sokoni pia wamekuwa wakizibiana riziki za tenda kama ilivyokuwa zamani.
KIVIPI?
Kwa mujibu wa ‘mtaalam’ wao mwenye kituo
cha kazi huko Yombo-Buza, Dar, wanachokifanya ni kufifisha na kuzimana
nyota hivyo kumpotezea mhusika mvuto kwenye jamii.
“Unajua kuna mastaa ambao walikuwa na majina makubwa sana lakini siku hizi siyo kama zamani.
“Baadhi wanawaroga wenzao kwa kuwasababishia matatizo ya magonjwa au
kwenye familia,” alisema mmoja wa wasanii waliokuwa waking’ara zamani
lakini siku hizi kafifia huku akimtolea mfano mwigizaji mmoja wa kiume
ambaye mkewe aliwahi kumkuta na hirizi.
Katika uchunguzi huo, baadhi ya mastaa walikuwa wakinyoosheana vidole
wao kwa wao huku listi ndefu ya mastaa wanaokesha kwa waganga
kuwamaliza wenzao ikianikwa (majina tunayo).
Ili kupata uthibitisho
wa uchunguzi huo, gazeti hili lilizungumza na baadhi ya vinara wa filamu
za Kibongo ambapo wengi walikiri kukithiri kwa ushirikina kwenye tasnia
hiyo.
JACOB STEVEN ‘JB’:
Sanaa yoyote ili idumu muda mrefu inahitaji baraka na neema ya Mungu.
Sisi tulianza enzi za Nyota Ensemble ‘Mambo Hayo’, baadaye ilikuja Kaole
Sanaa Group ndipo kukaibuka mapinduzi sisi tukashuka.
Mimi siamini mambo ya uchawi ila naamini katika kazi tu, wasanii waache kufanya kazi kimazoea.
Masuala ya kurogana mimi spendi kuyapa nafasi maana hayo kila sehemu
yapo, ninachoweza kusema ni kwamba wasanii wengi wa Bongo hawapo
‘siriasi’. JACQUELINE WOLPER: Mimi naamini sana
katika kazi lakini kwa kuwa Mungu ndiye kanipa jina hili, sina budi
kumshukuru yeye ila kama nimelipata kwa njia ya uganga basi nikose
kabisa.
ROSE NDAUKA: Uchawi ni ishu inayonisikitisha sana na
ukweli wapo mastaa wanafanya mambo hayo ili wapande. Mimi najua Mungu
hawezi kuwasaidia so nawashauri wafanye kazi, wasihangaike na uchawi kwa
sababu hauwezi kuwapandisha.
KAJALA MASANJA: Kusema kweli uchawi unatajwa sana
kwenye tasnia ya filamu Bongo hadi inanifanya kuamini hivyo kwa sababu
kuna watu kweli wakikuona unang’ara kwenye muvi watafanya kila wawezavyo
ili wakushushe tu na hasa kwa njia ya ushirikina.
SINGLE MTAMBALIKE ‘RICHIE’: Mimi asili yangu ni
Mwanza so kama ujuavyo watu wa Mwanza ni wachapa kazi, so nipo makini
sana na kazi yangu ya filamu na nipo kwenye tasnia kwa miaka 17 na
maisha yangu nayafanya ya kawaida tu wala sipendi kujikweza sana.
Kwa staili hiyo ningetumia nguvu za giza ningekuwa tajiri namba moja
hapa nchini maana siri ya kazi yoyote ni kuiheshimu na kujibidiisha. ELIZABETH MICHAEL ‘LULU’:
Tasnia yetu ya filamu naona kama hatuangalii mbali maana kwa wenzetu
wanashindana kikazi na si uchawi kama huku wanaofikiria kuwashusha
wenzao kisa wanaona wanafanya vyema, mimi ninachoweza kusema watu
wafanye kazi na wasibaki kuangalia nani anafanya nini na kumfanyia mambo
kama hayo yasiojenga maisha.
RUTH SUKA ‘MAINDA’: Mimi sijui sana kama kuna watu
wanafanya ushirikina. Ninachowaomba wamtegemee sana Mungu kwani
ninachoamini mimi kila kitu kipo kwa makusudi ya Mungu. Kama ukimroga
mwenzio ili ashuke basi hata wewe huwezi kufika mbali.
JACQUELINE PENTZEL ‘JACK CHUZ’:
Kweli mimi ninaumizwa sana na watu wanaotumia uchawi kuzima nyota yangu
kwa sababu kweli wapo wanaofanya hivyo tunawaona hata huko lokesheni
wanakamatwa na hirizi.
Wengine wanakutwa na matunguri ila mwisho wa siku naomba wajue kuwa
nyota na mafanikio ya mtu huletwa na Mungu na kujibidisha katika kazi
hivyo ninachoweza kuwashauri watu kama hao waachane na imani za
kishirikina.
SALUM HAJI ‘MBOTO’: Mimi ninachojua watu
wanatengeneza muvi kupitia migongo ya wenzao, unakuta mtu anatengeneza
sinema lakini anajua kabisa bila kumchezesha fulani hawezi kuuza hivyo
anatumia nyota ya mwenzake kuuza filamu yake.
AUNT EZEKIEL: Siamini sana katika kurogana ila
wanotumia njia hizo siamini kama wanafanikiwa kiasi hicho maana uigizaji
ni kipaji kutoka kwa Mungu na hakuna awezae kushusha kipaji hicho ila
najua uchawi upo na watu wanatumia uchawi kwenye mambo yao.
STEVE NYERERE: Uchawi haupo kwenye filamu tu hayo
yapo hata kwenye siasa. Watu kibao wanatembelea nyota za watu. Wapo
wanaoshinda kwa waganga, tunawajua ila cha msingi wafahamu kuwa hata
ukimfanyia mtu kitu gani huwezi kuwa staa.
SALOME NDUMBAGWE MISAYO ‘THEA’: Mimi ninaona kama
chalenji tu na kinyongo, maana wengi wanaotumia nguvu za giza hawachukui
muda mrefu wanashuka wao. Ninachoona mimi waachane na nguvu za giza
wamtegemee Mungu.
Baadhi ya waigizaji wengine waliowahi kurogwa na wenzao ni pamoja na
Wema Sepetu, Blandina Chagula ‘Johari’, Nuru Nassor ‘Nora’ na wengineo.