CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeibuka kidedea katika
uchaguzi wa Naibu Meya wa Jiji la Arusha, huku kikisisitiza msimamo
wake wa kutomtambua Meya wa jiji hilo, Gaudency Lyimo (CCM).
Ushindi wa CHADEMA ulikuwa wa mteremko baada ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM) kuacha kuweka mgombea huku mgombea wa Chama cha Tanzania Labour
(TLP), Michael Kivuyo naye akijitoa siku moja kabla ya uchaguzi.
Hata hivyo, mshindi wa kiti hicho, Diwani wa Kata ya Daraja Mbili,
Prosper Msofe, aliibua mzozo kwa madiwani wa CCM baada ya kutangaza
msimamo huo wa CHADEMA kutomtambua meya.
Uchaguzi huo ulifanyika jana wakati wa kikao cha mwisho wa mwaka cha
Baraza la Madiwani ambapo kulitanda ulinzi mkali wa polisi waliovalia
kiraia, Usalama wa Taifa na wale wa kutoka Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Kufanyika kwa uchaguzi huo, kumekata kiu ya wananchi wengi wa jiji
hili, hasa kwa kuzingatia kwamba nafasi hiyo imekuwa wazi tangu Desemba
2010 baada ya uchaguzi uliofanyika awali kwa kumweka madarakani Lyimo,
kudaiwa kuwa haukukidhi vigezo kisheria.
Hatua hiyo, ilimlazimu naibu meya aliyekuwa amechaguliwa kushika nafasi hiyo, Kivuyo (TLP) kujiuzulu.
Katika uchaguzi huo wa jana, Msofe aliibuka mshindi baada ya kupata
kura 25 za ndiyo na mbili za hapana huku moja ikiharibika hali
inayodhihirisha wazi kuwa madiwani wa CCM pamoja na wabunge wao nao
walimchagua.
Habari toka ndani ya kikao hicho, zinadai kuwa
mara baada ya Msofe kutangazwa kuwa naibu meya, alimweleza meya kuwa
hamtambui kwani taratibu zilizotumika kumweka kwenye kiti hicho hazikuwa
halali.
Akizungumza na Tanzania Daima nje ya kikao, Meya Lyimo
alikiri kutolewa kwa kauli hiyo huku akidai kuwa inashangaza kwani yeye
ndiye aliyesimamia uchaguzi uliomweka naibu meya huyo madarakani sasa
inakuwaje asimtambue.
Alisema kuwa hakuna uchaguzi mwingine wa
meya kwa sasa kwani sheria iko wazi kuwa uchaguzi hufanyika kila baada
ya miaka mitano wanapochaguliwa madiwani wengine.
Katika
uchaguzi wa kamati za kudumu za Mipango Miji, Mazingira na Ujenzi,
Diwani wa Moshono, Paul Matthysen (CCM) aliibuka mshindi kwa kupata kura
11 dhidi ya moja aliyopata Diwani wa Elerai, Injinia,Jeremiah Mpinga
ambapo kamati hiyo inaundwa na madiwani watano wa CHADEMA na sita wa
CCM.
Uenyekiti wa Kamati ya Uchumi, Elimu na Afya ulichukuliwa
na Diwani wa Ngarenaro, Doita Isaya (CHADEMA) aliyepata kura tisa dhidi
ya mbili alizopata Diwani wa Kata ya Engutoto, Elibariki Marlley
(CHADEMA).
Wakizungumza na waandishi wa habari, Matthysen
aliahidi kusimamia shughuli za kamati hiyo ipasavyo kwa kuhakikisha
watendaji wanazingatia sheria kwa kuhakikisha hakuna ujenzi holela
utakaoendelea kwenye Jiji la Arusha wala biashara zinazofanyika
pembezoni mwa barabara za waenda kwa miguu na magari.
Naye
Isaya aliahidi kufanya kazi kwa karibu na wanakamati wenzake pamoja na
wakuu wa shule ili kuhakikisha watoto wanapatiwa elimu bora sanjari na
kuwapunguzia wazazi mzigo wa michango mingi isiyo na tija.
Wakati huohuo, CHADEMA kimedai kuwa CCM haikusimamisha mgombea kwenye
nafasi ya naibu meya kwa kuhofia kushindwa kutokana na kuwa na idadi
ndogo ya madiwani.
CHADEMA walikuwa 15 huku wale wa CCM wakiwa 13 kutokana na mbunge wa viti maalumu, Namelock Sokoine kutohodhuria.