Dar es Salaam na mikoani. Wakati Serikali ikisisitiza kuwa huduma ya kumwongezea mgonjwa damu hospitalini ni bure, imebainika kwamba baadhi ya watu mitaani wakiwamo wabeba mizigo sokoni wanauza damu zao kwa watu wanaohitaji.
Mbali ya watu kuuza damu zao, majimaji hayo
mekundu muhimu mwilini yamegeuka bidhaa adimu baada ya baadhi ya wauguzi
na madaktari nao kugeuza huduma hiyo kuwa kitegauchumi chao.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii,
ni kosa kwa mtumishi yeyote wa afya nchini kumuuzia mgonjwa damu na wala
hakuna biashara ya kuuza damu kwa kuwa hutolewa bure na watu
wanachangia kwa hiari.
Uchunguzi wa kina uliofanywa na gazeti hili katika
hospitali mbalimbali nchini, umebaini hospitali nyingi hazina damu za
kutosha na hivyo kusababisha baadhi ya wagonjwa kuwalipa watu mitaani,
ili kuwatolea damu au kuinunua kwa wauguzi na madakari.
Hata hivyo, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa
Jamii, Dk Seif Rashid alisema kuwa wahudumu wa afya wanaoendesha vitendo
hivyo ni watu wanaojaribu kuizidi maarifa Serikali na kwamba wananchi
wamepewa taarifa za kutosha kuwa damu haiuzwi.
“Kuna watu wanajaribu kutuzidi maarifa, hiyo ni
tabia inayopaswa kupigwa vita. Mtu yeyote atakayetakiwa kununua damu,
atoe taarifa kwa mganga mkuu au kituo chochote cha polisi,” alisema.
Mkoani Dodoma
Wabeba mizigo wa soko la Majengo Mjini Dodoma,
wamekuwa mkombozi kwa wagonjwa wanaofika katika hospitali ya mkoa huo
baada ya kugeuza miili yao kuwa sehemu ya kuvuna damu na kuiuza kwa
ndugu wa wagonjwa hao.
Gharama za kuuza damu hiyo ni kati ya Sh10,000
hadi Sh30,000 kwa chupa moja, kutegemea na uwezo wa ndugu wa mgonjwa
huyo, lakini baadhi wamekuwa wakitoa zaidi kama sehemu ya shukurani.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili katika
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na kuthibitishwa na baadhi ya
wabeba mizigo hao, imebainika kuwa kitendo cha kutoa damu kwa wabeba
mizigo ni cha kawaida na kwamba utaratibu huo ulianza muda mrefu.
Enock Ayub ambaye ni mmoja wa watu ambao
wamechangia damu zaidi ya mara tatu kwa nyakati tofauti, alilimbia
gazeti hili kuwa biashara ya kutoa damu anaipenda na kwamba inampa
matumaini ya kuishi kwa kuamini kuwa bado ni mzima.
“Mimi nimechangia damu zaidi ya mara tatu, lakini
tukifika kule tunabadilisha majina maana madaktari wanataka mtu ukae
muda za miezi sita bila ya kutoa, sisi tunataka fedha ‘mkwanja’, hatuna
jinsi,” alisema Ayubu na kuongeza:
“Hata hivyo, napenda kutoa damu kwani ukiona wanakutoa ujue afya yako ni nzuri na huna Ukimwi na magonjwa mengine.”
Alipoelezwa hatari za kutoa damu mara kwa mara
bila kuzingatia ushauri wa daktari alisema, “Sioni tatizo maana fedha
tunazolipwa tunazitumia kunywa bia na matunda, hivyo afya zetu hurejea
kama kawaida, tena baada ya muda mfupi.”
Baadhi ya wodi ambazo gazeti hili lilitembelea na
kuzungumza na baadhi ya wagonjwa, lilibaini kuwa tatizo la damu katika
Hospitali ya Mkoa wa Dodoma limekuwa sugu, huku ndugu wa wagonjwa
wakilalamika kuwa wanauziwa damu kwa bei ya kati ya Sh40,000 hadi 60,000
kwa chupa moja.
“Mimi sitaki uniandike jina langu gazetini, lakini
ukweli ni kuwa madaktari walimpokea mgonjwa vizuri na damu aliwekewa
haraka sana tatizo likaja kwenye kuirudisha niliambiwa nitoe Sh60,000 au
mimi nitolewe damu, nilipogoma nikaonyeshwa Soko la Majengo kwa wabeba
mizigo,” anasema ndugu huyo.
Anasema kuwa alipofika kwa wabeba mizigo
walimuuliza daraja la damu aliyotoa na alipowatajia walijitokeza wawili
wenye daraja hilo wakaanza kupatana bei kabla ya kukubaliana na mmojawao
kwa kiasi cha Sh 25,000.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma,
Dk Nasoro Mzee, alikiri tatizo la damu ni kubwa katika hospitali hiyo na
kwamba linatokana na mwitikio mdogo wa wananchi katika kuchangia katika
benki ya damu.
Dk Mzee alisema hadi sasa kitengo hicho kina
upungufu wa damu na kwamba ni wanafunzi na askari tu ndio wanaochangia
damu kwa kiwango kikubwa.
“Wakifika watu ambao wana mahitaji ya haraka
tunachukua damu na kuwawekea, wengine ni kweli tunawaambia wachangiwe na
ndugu zao, na kwa wale waoga kutoa huwa wanakwenda kutafuta kwa
wanaojitolea kutoa damu,” alisema Mzee.
Alifafanua kuwa siyo kila damu inayotoka kwa mtu inakuwa salama kutumika, ni lazima ipimwe.
-mwananchi
-mwananchi