WATU
wanne wamekufa katika matukio manne tofauti jijini Dar es Salaam,
likiwemo la kukutwa maiti ya mtoto mchanga wa kike anayekadiriwa kuwa na
umri wa siku moja.
Kwa
mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke Engelbert Kiondo, maiti ya
mtoto huyo iliokotwa juzi saa 6:00 mchana katika maeneo ya Mtoni Relini
Dampo, ambapo ilikutwa imewekwa ndani ya mfuko wa plastiki na kutupwa
katika eneo hilo na mtu asiyefahamika.
Maiti
imehifadhiwa katika hospitali ya Temeke na upelelezi unaendelea.
Kamamda Kiondo alisema katika tukio jingine, watu wawili wamekufa katika
maeneo ya Mbande na Chamazi huku chanzo cha vifo vyao kikiwa
hakijajulikana.
Alisema
mkazi wa Mbande, Rashid Meso (26) akiwa katika biashara zake eneo la
Mbande alianguka ghafla na kufa akiwa njiani kupelekwa hospitali ya
Temeke.
Mtu
mwingine Juma Kasongo ambaye ni mchungaji wa ng'ombe wanaomilikiwa na
Donald Michael (39) ambaye alikutwa akiwa kitandani kwake akiwa
ameshakufa huku akitokwa na povu mdomoni.
Maiti
zimehifadhiwa katika hospitali ya Temeke kwa uchunguzi zaidi na
upelelezi unaendelea. Katika tukio jingine, Dia Haruna (6) amekufa baada
ya kugongwa na gari akivuka barabara katika eneo la Majohe, Wilaya ya
Ilala.
Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi alisema gari aina ya
Toyota Avensis yenye namba T 636 BYL ikiendeshwa na Njile Mlacha (39)
mkazi wa Majohe, akitoka kwa Diwani kwenda Kwa Mpogo alimgonga mtoto
huyo na kumsababishia majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake.
Majeruhi
alikufa muda mfupi baada ya kufikishwa katika hospitali ya Amana, maiti
imehifadhiwa hospitalini hapo na dereva wa gari hilo amekamatwa.