Zacharia Hans Poppe.
WEKUNDU wa Msimbazi Simba SC wamewataka mashabiki wao kuwa watulivu
wakati huu wa dirisha dogo la usajili kwani kamati iko makini kutafuta
wachezaji makini kwa ajili ya mzunguko wa pili wa ligi kuu soka Tanzania
bara.
Mwenyekiti wa kamati ya usajili wa klabu hiyo, kepteini wa zamani
wa jeshi la wananchi Tanzania (JWTZ), Zacharia Hans Poppe ameuambia
mtandao huu kuwa kwa sasa wanahangaikia nafasi ya mlinda mlango na nia
yao ni kusajili kipa mzawa kujiandaa na utarabu mpya utakaoanza kutumika
mwakani.
“Kama utaratibu mpya utaanza kutumika mwakani ambapo nafasi za
wachezaji wa kigeni ni tatu tu na kipa lazima awe Mtanzania., lazima
tutafute kipa mzawa ili kujiandaa na sheria hiyo mpya”. Alisema Poppe.
Poppe alisema tayari wameshapokea taarifa kutoka kamati ya ufundi
na leo hii watapata maono yao baada ya hapo na wao kamati ya usajili
wataingia kazini.
“Dirisha dogo tunahitaji wachezaji wawili au watatu ili kuongeza
nguvu zaidi, tumeona wachezaji wengi wa kusajili, lakini tutaangalia
maeneo muhimu zaidi kwa sasa ikiwemo nafasi ya mlinda mlango”. Aliongeza
Poppe.
Kepteini huyo wa zamani wa JWTZ aliwataka mashabiki wa Simba kuwa
na imani kubwa na viongozi wao kwani wanafanya kazi kwa weledi mkubwa
kwa malengo ya kuifikisha klabu mbali zaidi.
“Wapo wachezaji wengi wa kuwasajii, lakini mashabiki na wanachama
waelewe kuwa tunafanya kazi kuzingatia majukumu tuliyojipangia, hivyo
watuamini sana”. Aliomba Poppe.
Mwishoni mwa mzunguko wa kwanza, baadhi ya mashabiki wa Simba na
viongozi walitaka kumrejesha aliyekuwa mlinda mlango wao Juma Kaseja
Juma kwa madai kuwa kipa wao wa sasa, Mganda Abel Dhaira hana ubora
wanaoutaka wao.
Dhaira amekuwa katika wakati mgumu kutokana na shinikizo la kutaka
aondolewe, lakini kwa upande wake amekuwa akisisitizamkuwa yeye ni kipa
bora na kama anafanya makosa ni ya kawaida sana katika soka.
Lakini wamemkosa Kaseja aliyeitumia Simba kwa miaka 10 na mwishoni
mwa msimu uliopita alinyimwa mkatana mpya na kukosa mzunguko wa kwanza
wa ligi kuu kwani hakuwa na timu, ila kwa sasa ni jembe halali la Yanga
baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili kwa dau la milioni 40 za
Kitanzania.
Yanga SC wamemsajili Kaseja kutokana na uzoefu wake wa michuano ya
kimataifa ikizingatiwa kuwa mwkaani wao ndio wawakilishi wa Tanzania
katika michuano mikubwa ya klabu bingwa barani Afrika .