Mfanyabiashara wa magari, Gabriel Munisi
(35), jana alijiua baada ya kumuua mtu mmoja na kujeruhi wengine watatu
jijini Dar es Salaam katika tukio linalohusishwa na wivu wa mapenzi.
Munisi, ambaye alikuwa mkazi wa Mwanza,
aliwapiga risasi watu watatu akiwamo mchumba wake, Christina Alfred
katika Mtaa wa Bungoni Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam.
Baada ya kumpiga risasi mchumba wake
huyo na kudhania kwamba amemuua, inadaiwa kwamba Munisi aliendelea
kuwamiminia risasi watu wengine na kumuua mdogo wake Christina, Alpha
(22).
Katika tukio hilo, Christina na mtu
anayedaiwa kuwa mchumba wake mpya, Francis Shumila wamelazwa katika
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili baada ya kujeruhiwa. Mama yake
Christina, Helen Alfred amelazwa katika Hospitali ya Amana baada ya
kujeruhiwa pia.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marieta
Minangi alisema Munisi alikutwa na bastola moja, magazini mbili na
yalikutwa maganda 14 ya risasi zilizotumika na risasi mbili ambazo
zilikuwa hazijatumika.
Tukio hili limetokea mwezi mmoja baada
ya mwandishi wa habari wa ITV, Ufoo Saro kujeruhiwa kwa risasi na mzazi
mwenzake, Anthery Mushi.
Katika tukio hilo, Mushi alijiua baada
ya kumuua mama mzazi wa Ufoo na inaaminika pia tukio hilo lilisababishwa
na masuala ya mapenzi.
Lilivyotokea
Mashuhuda waliokuwapo katika tukio hilo
walisema mauaji hayo yalitokea saa 1.15 asubuhi baada ya Munisi kufika
Ilala Bungoni na kwenda katika Klabu ya Wazee iliyo jirani na eneo
yalipotokea mauaji na kunywa supu kabla ya kusogea karibu na lango la
nyumba anakoishi mchumba wake.
Mmoja wa majirani, Noel Gerald alisema alimuona Munisi akiwa amesimama karibu na lango la nyumbani kwa kina Christina.
Alisema baadaye waliona gari aina ya
Toyota Hilux, Surf, likitoka katika lango la nyumba hiyo na mara
walimuona Munisi akimwamuru dereva ashushe kioo lakini alikataa na kudai
kwamba ndipo alipoamua kuwapiga risasi waliokuwamo kwenye gari hilo.
Alidai kuwa Munisi alipiga risasi nane
mfululizo huku akiwa analizunguka gari hilo na kwamba alimpiga dereva
ambaye baadaye alifahamika kuwa ni Shimula. Imeelezwa kuwa majeruhi huyo
ni raia wa Kenya na ni rubani wa ndege.