Search in This Blog

TFF YAIOMBA MANCHESTER UNITED ICHEZE DAR

Dar es Salaam. Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amemwomba Meneja Uhusiano wa Manchester United, Michael Higham kuufikishia salamu uongozi na benchi zima la ufundi la Manchester United kuwa TFF inaitaka klabu hiyo kutembelea Tanzania.
Malinzi aliyasema hayo jana kwenye hafla ya uzinduzi wa ushirikiano kati ya klabu hiyo na Kampuni ya Simu za Mkononi ya Airtel hasa katika maendeleo ya soka ya vijana.
“Ukifika England, waambie wakubwa, benchi la ufundi kuwa tunawaalika Tanzania kucheza mechi moja, pia kuna mambo mengi ya kuona huku kuna Mbuga za Wanyama Serengeti, Selou, Manyara, Mlima Kilimanjaro kuna mengi ya kuvutia,” alisema.
Alisema kuwa kuja kwa timu hiyo itakuwa funzo zuri kwa maendeleo ya soka kwani vijana watataka kuiona ‘live’ na watacheza kama wanavyocheza wao.
“Walikuwa Afrika Kusini, waliwahi kwenda Nigeria na hata Tanzania wanaweza kuja...waje,” alisema Malinzi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Michezo, Leonard Thadeo alisema hatua ya Manchester United kuunga urafiki na Airtel itasaidia kwa kiasi kikubwa kudumisha maendeleo ya soka  ya Tanzania kwa vijana.
“Ni nafasi ya Tanzania kujifunza aina ya soka ya England kwani walishaanzisha mpango wa Airtel Raising Stars ambao unatengeneza vipaji kwa vijana...naomba TFF na wadau wengine kuendeleza vijana hawa.
“Lakini pia mwaka 2015 ni uchaguzi, tuitumie soka hiyo hiyo kudumisha amani na umoja kwa Watanzania na kwamba Serikali itakuwa bega kwa bega na TFF katika kushughulikia maendeleo ya soka,” alisema.
 
Support : KARIBU TENA MDADISI MAM
Copyright © 2011. RISASI - Haki Zote Zimehifadhiwa.
KWA HISANI YA MDADISI MAMBO
Proudly powered by Blogger