Akisimulia tukio hilo, kaka wa mwanamke huyo aliyejitambulisha kwa jina la Mbwana, alisema tukio hilo lilitokea asubuhi ya Julai 6, mwaka huu, wakati akienda msalani aliposikia sauti ya kichanga ikilia kutoka chumbani kwa dada yake, hali aliyoiona siyo ya kawaida kwani hakuwa na mtoto.
Kuona hivyo, alisema alikwenda na kugonga mlangoni kwa dada yake huyo, lakini hakufungua mpaka alipoamua kuvunja mlango. Cha kushangaza, alisema alimkuta akiwa kama aliyechanganyikiwa, akijifanya kufagia huku damu zikiwa zimetapakaa ndani.
Baada ya hapo, ndugu hao walikwenda kutoa taarifa katika kituo kidogo cha polisi Keko Machungwa na mtuhumiwa pamoja na kichanga chake walipelekwa katika Hospitali ya Polisi Barracks iliyopo Kilwa Road.
DAKTARI ATHIBITISHA
Daktari wa hospitali hiyo, Ahamed Said alithibitisha kupokea kichanga hicho chenye jinsi ya kike kilichozaliwa siku hiyohiyo ambapo uchunguzi ulionyesha kwamba mguu wake wa kulia ulikuwa umevunjika vibaya, kiasi kwamba ulikuwa ukizunguka kama feni.
Alisema mtoto alikuwa katika hali ya kukosa hewa na kukubaliana na madai ya kaka wa mwanamke huyo kwamba alikuwa katika jaribio la kuutoa uhai wa kiumbe huyo.
MTUHUMIWA AZUNGUMZA
Akizungumza ndani ya wodi ya wazazi, Fadhila alisema kwamba tukio hilo lilikuwa la bahati mbaya na huyo ni mwanaye wa nne, akidai wengine wanaishi kwa baba yao ambaye waliachana akiwa na ujauzito huo kutokana na kushindwa kuelewana.