Utata umeibuka kuhusiana na kifo cha Ofisa Usalama wa Taifa, Peter Tyenyi, ambaye mwili wake umekutwa ndani ya kisima cha maji kilichopo eneo la ofisi za idara zilizopo Kijitonyama, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kwa njia ya simu,
msemaji wa familia ambaye ni kaka wa marehemu, John Tyenyi alisema mwili wa
Peter (53) ulikutwa juzi ukiwa ndani ya kisima cha maji kilicho ndani ya eneo
la Ofisi za Usalama wa Taifa, Kijitonyama baada ya kutoweka tangu Jumatatu ya
Mei 27, alipoaga kwenda kazini.
“Peter alitoweka tangu Jumatatu
alipoaga kwenda kazini. Mimi nimepigiwa simu jana saa tano asubuhi nikiwa
Mombasa nchini Kenya kwamba amepatikana akiwa ndani ya shimo la maji,” alisema
John.
Baadhi ya ndugu zake waliozungumza
kwa sharti la kutotajwa majina wakiwa msibani Kigamboni jijini Dar es Salaam,
walisema kuwa baada ya ndugu yao kutoweka mkewe Joyce Mwakilama aliwataarifu na
kuwasiliana na ofisi yake, lakini aliambiwa kuwa hata huko hayupo.
“Tuliwajulisha Usalama wa Taifa
wakasema hata wao hawajui. Lakini jana (juzi) wakatupigia simu kuwa amekutwa
kwenye kisima cha maji baada ya kutokea shida ya maji,” alisema mmoja wa
wanafamilia kwa sharti la kutotajwa jina na kuongeza:
“Walisema kuwa kisima hicho huwa
kinalindwa, lakini tunashangaa ndugu yetu aliingiaje humo.” Ndugu mwingine
alisema: “Awali tuliambiwa kuwa ndugu yetu yuko Muhimbili, tukaenda kuulizia
tukamkosa. Baadaye tukaambiwa yuko hospitali ya Lugalo, huko tukamkuta
ameshaandaliwa kwa mazishi. Tulipouliza tukaambiwa kibali cha kuzika kiko
tayari na usafiri wa ndege uko tayari tujiandae kusafirisha.”
Hata hivyo, msemaji wa familia John
Tyeni alisema kuwa ndugu hao walipinga kuusafirisha mwili huo, hadi ufanyiwe
uchunguzi (post mortem).
“Tulipokwenda hospitali tukakuta
maofisa usalama wamemchukua OCD wa Wilaya ya Kinondoni Wilbrod Mutangungwa na
askari wawili na kwenda kufanya post mortem. Yaani kulikuwa na ujanja ujanja
unafanyika. Sisi tukamchukua Ofisa Upelelezi Mkoa wa Kinondoni, RCO Kimola na
askari wawili na wapigapicha ndiyo tukafanya post mortem,” alisema John.
Akizungumzia matokeo ya uchunguzi
huo, John alisema kuwa watapewa matokeo hayo baada ya kutoka kwenye mazishi
yatakayofanyika Musoma mjini mkoani Mara, baada ya kusafirishwa leo.Hata hivyo
alisema kuwa macho yake yalikuwa yametoka nje kwa sababu ya kujaa maji.
Baadhi ya ndugu wa marehemu walidai
kuwa mwili wake ulikutwa ukiwa umetumbuliwa macho huku
nguo na viatu vikiwa bado mwilini. Akizungumzia kifo hicho, Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela alikiri kutokea tukio hilo na kusema kuwa
bado uchunguzi unaendelea.
“Ni kweli kuna ofisa usalama amefariki ndani ya kisima, lakini bado tunachunguza. Kwa sababu itabidi tupate taarifa ya daktari ndiyo tuunganishe na uchunguzi wetu,” alisema Kenyela.
“Ni kweli kuna ofisa usalama amefariki ndani ya kisima, lakini bado tunachunguza. Kwa sababu itabidi tupate taarifa ya daktari ndiyo tuunganishe na uchunguzi wetu,” alisema Kenyela.