SIKU chache baada ya Balozi wa China nchini, Lu Youqing,
kukiuka mkataba wa kimataifa wa Vienna kwa kushiriki kazi ya uenezi wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM), Tanzania Daima limedokezwa kuwa kuna
harakati za kumrudisha nyumbani kwao.
Septemba 12 mwaka huu, balozi huyo alihudhuria mkutano wa hadhara wa
CCM uliofanyika uwanja wa Shycom mkoani Shinyanga na baadaye katika
eneo la mnada wa Mhunze Jimbo la Kishapu.
Balozi Youqing alitambulishwa kwa wananchi waliofika kwenye mkutano
huo na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, na alihutubia akisema
China imevutiwa na sera za chama hicho na hivyo itawekeza katika soko
la pamba katika mkoa huo.
Tanzania Daima limedokezwa kuwa tukio hilo limeitia doa Serikali ya
China ambayo licha ya ‘urafiki’ na Serikali ya CCM, imekuwa ikilaumiwa
kwa kukiuka haki za binadamu na mataifa mbalimbali ulimwenguni.
Balozi huyo amezusha maswali mengi miongoni mwa jamii juu ya uelewa
wake wa masuala ya kimataifa, hasa mkataba Vienna wa mwaka 1961 kifungu
cha 41(1) kinachozungumzia uhusiano wa kidiplomasia.
Kifungu hicho kinazuia balozi yeyote kujihusisha na siasa kwenye nchi anayofanyia kazi.
Tanzania Daima limedokezwa kuwa katika mkutano huo, balozi huyo
alicheza nyimbo za CCM za kubeza vyama vya upinzani huku akiwa amevalia
kofia ya chama hicho tawala.
Wachambuzi wa masuala ya diplomasia wamekuwa na mtazamo wa aina mbili
juu ya tukio hilo lililotia doa Serikali ya China na CCM.
Mtazamo wa kwanza ni kuwa viongozi wa CCM wakiongozwa na Kinana
walilenga kumtumia balozi huyo kutafuta uungwaji mkono na wananchi wa
Shinyanga.
Wanabainisha kuwa balozi huyo ameingizwa ‘mkenge’ na CCM
inayojipatatua kurejesha imani yake kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa ambao
wanaonekana kuviunga mkono vyama vya upinzani.
Mtazamo wa pili wa wachambuzi hao ni juu ya elimu na uzoefu wa balozi
huyo katika masuala ya kimataifa kiasi cha kushindwa kubaini kile
alichokuwa akikifanya ni kosa.
Tanzania Daima iliwasiliana na maofisa wa ubalozi wa China nchini juu
ya hatua atakazochukuliwa balozi huyo, lakini hawakuwa tayari
kuzungumzia jambo hilo.
Ofisa mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alisema
mzungumzaji wa masuala ya kibalozi ni balozi ambaye hayupo tayari
kulizungumzia.
Licha ya ubalozi huo kutokuwa tayari kulizungumzia, Tanzania Daima
imedokezwa kuwa kuna fununu za balozi huyo kurejeshwa nyumbani kwao.
Inadaiwa ushiriki wa balozi huyo kwenye shughuli za CCM umewashtua
mabalozi wengine ambao wameweka wazi kuwa kabla ya kupangiwa vituo vyao
vya kazi hupewa mafunzo maalumu ya mambo ya kufanya pamoja na mikataba
ya kimataifa.
Ilivyokuwa
Septemba 13, mwaka huu Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CHADEMA, Ezekia
Wenje, alipinga balozi huyo kushiriki kwenye majukwaa ya kisiasa na
kuvaa sare za CCM.
Wenje alisema balozi huyo amekiuka mkataba wa kimataifa wa Vienna kuhusu mambo ya kidiplomasia kifungu cha 41 (i).
Alisema kifungu hicho kinakataza mabalozi wa nchi kujiingiza katika masuala ya ndani ya nchi nyingine.
Wenje alibainisha kuwa mkataba huo unataka kazi za balozi kuwa ni kuwakilisha nchi na si chama.
“Balozi wa China yuko hapa kuwakilisha China nchini Tanzania, si Chama cha Kikomunisti kwa CCM,” alisema.
Hata hivyo Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC) Itikadi na Uenezi wa CCM,
Nape Nnauye alisema kuwa ziara ya balozi huyo mkoani Shinyanga haikuwa
ya kisiasa bali ilitokana na mazungumzo kati ya chama hicho na Chama
cha Kikomunisti cha China.
Alisema kuwa lengo lilikuwa ni China kuweza kuwekeza katika kilimo cha pamba na mifugo kuongeza ajira.
“CHADEMA kulalamika ni kwamba wameweweseka kwa kuwa wamezoea kutumia
matatizo ya wananchi kama mtaji wa kisiasa, tatizo la bei ya pamba
likiendelea ni mtaji kwao na likiisha watakosa mtaji wa kisiasa,”
alisema.
Wizara yampinga
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, ilitoa taarifa
iliyosainiwa na Togolani Mavura kwa niaba ya waziri wa wizara hiyo,
Benard Membe kuwa alichokifanya balozi huyo si sahihi.
Aliongeza kuwa wizara inapenda kutamka kwamba kitendo cha balozi
yeyote kuhudhuria mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa na kuvaa sare
zenye nembo ya vyama sio sahihi. Ni kukiuka kifungu cha 41(1) cha
mkataba wa Vienna wa mwaka 1961, unaoongoza uhusiano wa kidiplomasia.
“Katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2012 wizara ilikumbana na vitendo
vinavyofanana na kitendo hiki na ikachukua hatua stahiki.
“Kadhalika kwa tukio hili, waziri anakusudia kuchukua hatua za
kidiplomasia zinazostahili ili kuzuia jambo hili lisitokee tena,”
alisema.
Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi naye amepinga
kitendp cha balozi huyo na kuahidi kuwa kuanza sasa atakuwa mkali kwa
vyama vinavyokiuka mikataba mbalimbali katika kuendesha shughuli zao.
-Tanzania Daima