BINTI WA MIAKA 6 ABAKWA NA MFUGA NGURUWE HUKO KITUNDA BAADA YA KUMRUBUNI KWA KUMNUNULIA PIPI.
PEPO la ubakaji linazidi kutikisa jamii ambapo hivi karibuni watoto wawili wanaripotiwa kubakwa kwa nyakati tofauti jijini Dar.
Mtoto mmoja, mkazi wa Kitunda (jina linahifadhiwa) amebakwa na mfanyakazi wa kufuga nguruwe aishie maeneo ya jirani baada ya kumrubuni binti huyo mwenye umri wa miaka 6 kuwa atamnunulia pipi.
Akizungumza kwa uchungu, baba wa mtoto huyo, Joseph Isaac alisema mwanaye alibakwa na mfanyakazi huyo wa nguruwe aliyemtaja kwa jina la Fabiano baada ya kumuahidi kuwa atampa pipi.
“Siku hiyo nilirudi nyumbani nikamkuta mwanangu anachemka homa kali, nikamwambia mama yake amuogeshe tumpeleke hospitali kwani tulikuwa tumeshampatia dawa ya kutuliza lakini haikumsaidia,” alisema baba huyo.
Mama wa mtoto huyo aliyetajwa kwa jina la Elizabeth, alimuogesha mwanaye na kugundua kuwa alikuwa amevimba sehemu za siri kutokana na majeraha aliyopata na alipombana ndipo alipomtaja mfanyakazi huyo wa nguruwe.
“Nilimwambia mume wangu tukachukue PF3 (fomu ya uthibitisho wa polisi) kisha tukatibiwe. Tulienda Kituo cha Polisi Stakishari na kuandikisha RB No KIT\RB\2804\2013 KUBAKA ndipo tukaenda Hospitali ya Amana kwa ajili ya matibabu,” alisema mama huyo.
Walipofika katika Hospitali ya Amana, walilazimika kulazwa kwa siku tatu kutokana na majeraha makubwa aliyokuwa nayo mtoto huyo wakati huohuo polisi walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa (Fabiano).
Ilielezwa kuwa, pamoja na mtuhumiwa kukamatwa lakini alitolewa kwa dhamana hivyo wazazi wa mtoto huyo kuhoji kulikoni aachiwe.
Waandishi wetu walikwenda kwa mjumbe wa eneo hilo, Anna Kosmas ambaye alikiri kutokea kwa tukio hilo na kuambatana na waandishi hadi nyumbani kwa mtuhumiwa ambapo walielezwa kuwa ametoweka.
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Ilala, Marietha Minangi aliahidi kufuatilia suala hilo kwani limesharipotiwa kituoni hapo na atahakikisha mtuhumiwa anakamatwa.
Unyama haukuishia hapo, mtoto mwingine mkazi wa Makabe, Dar aliyejulikana kwa jina la Sara (10) amesimulia jinsi alivyokuwa akibakwa mara kwa mara na mlinzi wa baa anayejulikana kwa jina la Athuman.
Akizungumza kwa masikitiko, mtoto huyo alisema kila siku huwa anaenda kuangalia video kwenye Pub ya Jack anayolinda mlinzi huyo ambapo wakati wa kurudi inakuwa ni usiku ndipo mlinzi huyo anapotumia muda huo kumaliza haja zake.
Alisema mlinzi huyo alikuwa akimkamata kwa nguvu na kumfunga kamba mkononi, miguuni na kumziba mdomo huku akimtishia kuwa akipiga kelele, atamchoma mkuki kitendo ambacho kilimsababisha mtoto aogope kumwambia hata mama yake.
Hata hivyo, imeelezwa kuwa baada ya kugundulika kwa mchezo huo mchafu, polisi walimkamata mtuhumiwa na kumfikisha katika Kituo cha Polisi cha Kwa Yusuf, Mbezi Beach, jijini Dar kukamilisha taratibu za kipolisi kisha kumpeleka mahakamani.