CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimemtaka
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa kujiuzulu kwa
kushindwa kulipa madeni ya walimu nchini.
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana
pia ametoa muda wa miezi sita kwa Waziri huyo na Naibu wake Philip
Mulogo kutekeleza hilo agizo hilo vinginevyo chama kitawatumia wabunge
wake kuwatimua kwa nguvu.
Kwa mujibu wa taarifa za madeni
zilizokusanywa na Chama cha Walimu Tanzania (CWT), hadi sasa walimu
wanadai malimbikizo yao ya Sh bilioni 49 ambayo hajalipwa na Serikali.
Kinana alikuwa akihutubia mikutano ya hadhara jana katika wilaya za Bariadi na Busega.
Alisema CCM haiko tayari kuona walimu wakinyanyaswa wakati wana madai ya msingi.
Hivi sasa imejengeka tabia kwa baadhi ya
mawaziri na watendaji wa wizara ya kuwadharau walimu na hata
kuwanyanyasa huku wengine wakishusha utu na heshima ya walimu kwa
kuwatukana, alisema.
Kinana ambaye yupo katika ziara ya mikoa
ya Kanda ya Ziwa alisema kwa mawaziri kushindwa kutatua kero za walimu,
imefika wakati wahusika waondoke wenyewe na wasipofanya hivyo chama
kitawaagiza wabunge wake wawafukuze kwa nguvu.
“Ninatoa muda wa miezi sita kwa Waziri
wa Elimu na wasaidizi wake wakiwamo watendaji kuhakikisha wanalipa
madeni ya walimu haraka. Haiwezeni hii ni nchi ya watu wote wakiwamo
walimu wadharauliwe na hata kunyanyaswa kwa maneno ya matusi
“Hili hapana
CCM haiko tayari kuona walimu kila siku wakipigwa danadana kutokana na
uzembe wa watu waliokabidhiwa dhamana za kuongoza sekta ya elimu katika
nchi yetu,” alisema.
MTANZANIA ilimtafuta Katibu Mkuu wa CWT,
Ezekiah Oluoch ambaye alisema hadi sasa madeni ya walimu yamefikia Sh
bilioni 49 ambayo ni malimbikizo ya mishahara na mapunjo.
“Kila mara
tunawaambia kuwa ni vema Serikali itafute Sh bilioni 100 katika fungu la
dharura ili iweze kulipa madeni ya walimu na iachane nao lakini
hawasikii,” alisema Oluoch.
SOURCE MTANZANIA