Msanii wa muziki wa bongo fleva ambaye
sasa ni mjasiriamali pia Anasteria Sanga Linah au muite Ndege Mnana
amefunguka kuwa producer wa studio ya Bhitz Pancho Latino ndiye mwenye
siri nzito ya penzi lake na msanii mwenzake Amini ambaye kwasasa penzi
lao limekuwa stori ya kale baada ya kuachana.
Linah amesema tokea wanaanza mapenzi yao
Pancho ndiye alikuwa mtu pekee anayejua mambo mengi kuwahusu wao na
jinsi walivyotumbukia katika penzi ambalo anasema yeye binafsi ndiye
hasa alikuwa akimpenda Amini kupita kiasi japo baadaye akagundua kuwa
hata mwenzake naye anamzimika na hivyo penzi likawa linasonga.
"Yaani we muulize Pancho yule ndio ana
siri kubwa sana ya penzi langu na Amini,yaani jamani nilimpenda sana
Amini mpaka nikakubali kuingia kwenye mapenzi na nilimpenda hasa kutoka
moyoni,kuna vitu vingi nyuma yake ambavyo Pancho anajua",alisema Linah.
Msanii huyo mwenye sauti tamu kiasi cha
kupachikwa jina la Ndege Mnana na msanii mkongwe Patricia Hillary
ameendelea kufunguka kuwa wakati ameangukia katika penzi la Amini
alikuwa anawachomolea wanaume wengi waliokuwa wanamtokea tena wenye pesa
zao na wengine ni watu wazito lakini aliamua kutoka moyoni kwa dhati
kuwa na Amini kwahiyo akawa anamtunzia heshima yake.
Anasema kama angekuwa macho juu kuna
uwezekano mkubwa asingeendelea kuwa na Amini au angekuwa anamsaliti kwa
kiasi kikubwa lakini moyo wake usio na tamaa ndio ulikuwa unamfanya
aendelee kumpatia penzi la kweli.
Akavujisha siri kuwa Amini ndiye
aliyemtibua na ndipo akapitisha uamuzi wa kujiweka pembeni kwasababu
ambazo ni ngumu kuziweka hadharani lakini mpenzi wake huyo wa zamani
anazijua na ni sababu ambazo haziwezi tena kulirudisha penzi lao japo
anakiri kuwa aligundua kuwa mpenzi wake huyo wa zamani anampenda siku
alipomtamkia kuwa mapenzi yameisha kila mmoja ashike lake.
Anasema katika kuonesha kuwa ameachana na Amini lakini hana bifu naye wakaamua kutoa wimbo wa pamoja wa Mtima wange.
Akizungumzia show anazofanya na Amini
jukwaani wakiwa kama wapenzi anasema ni kuonesha kuwa hakuna bifu na
hata mabusu anayopigwa na zilipendwa wake huyo anayapokea kwasababu
anashindwa kuyapotezea jukwaani akiogopa kumtia aibu jamaa huyo mbele ya
mashabiki na watu wengine.