Serikali kupitia Waziri wa Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, imesema kuwa kitendo
kilichofanywa na Balozi huyo siyo sahihi na kinakiuka mkataba wa Vienna.
“Wizara inapenda kutamka kwamba kitendo
cha Balozi yoyote kuhudhuria mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa na
kuvaa sare zenye nembo ya vyama vya siasa siyo sahihi na kinakiuka
Kifungu cha 41(1) cha Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961, unaoongoza
uhusiano wa kidiplomasia,” alisema Membe katika taarifa yake jana jioni.
Taarifa hiyo ilisema kuwa mkataba huo
unazuia wawakilishi wa nchi za nje kujihusisha na ushabiki wa kisiasa
wanapofanya kazi zao kwenye nchi za uwakilishi.
“Katika kipindi cha mwaka 2010 hadi
2012, Wizara ilikumbana na vitendo vinavyofanana na kitendo hiki na
ikachukua hatua stahiki, kadhalika kwa tukio hili Wizara itachukua hatua
za kidiplomasia zinazostahili ili kuzuia jambo hili lisitokee tena,”
alisisitiza.
Taarifa hiyo ilisema kuwa Balozi huyo
alikwenda wilayani humo kuhudhuria uzinduzi wa mradi wa viwanda vya
kuchambulia pamba vinavyojengwa na mwekezaji wa Kichina anayeitwa
Tahong, na viwanda hivyo vitakuwa na uwezo wa kuchambua tani 120,000 za
pamba kwa mwaka, vitakapokamilika mwakani.
Alisema Wizara imeona picha na habari kwenye vyombo vya habari zikieleza na kumuonyesha Balozi huyo akiwa kwenye mkutano wa CCM.
ALICHOSEMA BALOZI
Balozi huyo amenukuliwa na vyambo vya
habari wakati akihutubia mkutano wa hadhara akiwa na Katibu Mkuu wa CCM,
Abdulrahman Kinana, na kujitahidi kuwasalimia wananchi hao kwa lugha ya
kabila la Wasukuma kwa kusema mwadila.
Alisema pamoja na Tanzania kuwa na mfumo
wa vyama vingi, anaamini kuwa CCM bado iko imara na inaweza kuendelea
kuongoza kwa muda mrefu.
“Kwa hili inadhihirisha kuwa hakuna
chama kama CCM kutokana na uimara wake na hili wanalofanya sasa la kuja
kuimarisha chama nasi kule China kupitia chama chetu tawala cha CPC
(Chama Cha Kikomunisti cha China), tunafanya kama hivi pia. Mwadila,
Shinyanga, CCM Oyeeeeee asanteni sana,” alikaririwa akisema.
Source:Nipashe Jumanne