Mwandishi wa kike, Galaletsang Molabi wa blog changa ya Botswana, 1980sumn ameandika makala kumtaka Feza Kessy arudi nyumbani kutumia jina alilolipata baada ya kushiriki shindano la Big Brother Brother The Chase.
“Lini Feza ataenda nyumbani kuutumia umaarufu wake wa BBA?” anauliza mwandishi huyo.
“Siulizi swali hili kwasababu mimi ni hater wa ‘Oneza’ kama wengine wanavyoweza kuhisi. Nauliza kwasababu, ndani yangu kama mfanyabiashara, napenda afanikiwe.”
Molabi anasema inamshangaza hadi sasa kuona Feza hayupo kwao (Tanzania) kutumia umaarufu wake kujikuza kimuziki.Amesema hivyo kwasababu, mpenzi wake Oneal amekuwa akitengeneza hela nzuri baada ya shavu la BBA ambapo amekuwa akipata mialiko kwenye club nyingi hata za Afrika Kusini kama Dj.
Anauliza pamoja na Feza kuwa pembeni ya Oneal muda wote, mpaka sasa hawajaweza kupata show na kutumbuiza ama kwa kulipwa kutokana na appearance yake sehemu. Mwandishi huyo anasema alitegemea kuona Feza anatumia muda huu nyumbani kupromote zaidi wimbo wake lakini ameendelea kukaa Botswana wakati Oneal akilikuza tu jina lake.
“Nafikiria tu kiasi cha fedha ambacho angekuwa akikiingiza sasa hivi kwa kutumbuiza nyimbo zake kwa watu wa nchi yake, kuendeleza career yake ya muziki wakati chungu cha BBA kingali cha moto,” anasema.
“Kwa upande mwingine, vipi kuhusu mashabiki wake wa Tanzania? Lini watapata nafasi ya kumshangilia. Walimpigia kura, walimuunga mkono na tunaweza kuhisi kuwa walikuwa wakingoja kwa hamu kumuona nyota wao. Bahati mbaya hawakuweza kupata nafasi hiyo kutoka kwake. Hao ni watu walio nyuma yake. Naamini penzi lingesubiri kwa miezi mitatu. Penzi linaweza kuishi lenyewe hivyo umbali sio issue hapa.”
“So if you see sweet beautiful Feza on the streets of Gabs, please tell her to ‘go home Fezaaaa,” alimalizia mwandishi huyo.
Mtazamo wangu
Kwa namna fulani mwandishi amezungumza masuala ya muhimu ambayo Feza anahitaji kuyazingatia japo ntaeleza pia ni kwanini ni sahihi kwa Feza kuwa Botswana.
Kwanini Mwandishi ana point:
Ni kweli baada ya Feza Kessy kurudi kutoka Big Brother, hajawapa nafasi ya kutosha mashabiki wake kumfahamu zaidi.
Alipochaguliwa Big Brother, Feza Kessy hakuwa na jina kubwa kihivyo. Waliokuwa wakimfahamu ni wale waliofuatilia mashindano ya Miss Tanzania, mwaka 2005/2006 alipokuwa Miss Dar City Center. Kwa wengi, Feza Kessy lilikuwa jina geni kabisa. Na hata jina lake lilipotajwa kuwa ataiwakilisha Tanzania kwenye shindano hilo, wengi waliuliza ‘Feza ndio nani?’ Kwa muda mfupi baada ya kukaa wiki chache tu kwenye jumba la Big Brother, jina lake likawa kubwa na tayari akaingia kwenye klabu ya mastaa wa Tanzania. Ni kweli, Feza alikuwa mshiriki mwenye nguvu kwenye The Chase na Afrika ilimpenda.
Alipokuja Tanzania baada ya kuondolewa, alipaswa kutumia muda kuconnect na mashabiki wake kwa namna nyingi. Ikumbukwe kuwa video ya wimbo wake Amani ya Moyo, ilitoka wakati tayari yupo BBA. Maana yake ni kuwa, alipaswa kuipromote baada ya kuja, hasa kwa kufanya interview nyingi za TV, kama kweli muziki ndicho kitu anachotegemea kimwekee chakula mezani (aliwahi kusema hivyo). Hata hivyo, muda na nafasi wa kufanya hili bado upo.
Naamini pia, kama angekuwa Tanzania, huenda angepata shavu la kutumbuiza kwenye baadhi ya show za Fiesta ama Kili Tour, ingewezekana kabisa.
Kwanini Feza Kessy yupo sahihi kukaa Botswana?
Kuweka mizizi ya penzi lake na Oneal
Hakuna ubishi kuwa, wakiwa na penzi changa mikononi mwao, Oneal na Feza walihitaji muda wa haraka kujuana zaidi nje ya maisha ya Big Brother ambayo kwa kiasi kikubwa yalikuwa nusu kweli na nusu kuigiza. Imani ya Molabi kuwa ‘mapenzi yangesubiri kwa miezi mitatu’ haina uhalisia. Kabla hata ya Oneal kwenda BBA, jina lake nchini Botswana lilikuwa kubwa na baada ya kurejea kutoka BBA, limekua maradufu. Hiyo ina maana kuwa, Oneal alijikuta yupo katikati ya vishawishi vingi kutoka kwa wasichana wengi warembo wanaotaka nafasi kwenye moyo wake. Ilikuwa ni muhimu Feza ajuane na Oneal mapema iwezekanavyo kisha mengine ndio yafuate. Ilikuwa muhimu kwake kwenda kuweka ngome nzito kulilinda penzi la Oneal.
Malengo ya Feza Kessy ya kuwa mwanamuziki wa kimataifa
Baada tu ya Feza kutoka BBA, alihama kutoka kuwa muimbaji wa Tanzania pekee na kuwa muimbaji mwenye sura ya Afrika.
BBA imempa exposure kubwa zaidi ambayo hatakiwi kuitumia Tanzania tu. Na kwa muziki wa Feza, kama akitegemea soko la Tanzania tu, si rahisi ukampa kile anachotaka (tunajua aina ya muziki unaofanya vizuri kiuchumi Bongo).
Ni vizuri anapokuwa Botswana kwa mchumba wake kwakuwa tayari anakuwa jirani na kitovu cha muziki wa Afrika, Afrika Kusini. TV zote kubwa za Afrika ziko huko. Akiwa jirani na huko, ni rahisi kwake kupata endorsements za ukweli na hata mashavu mengine makubwa, kuliko akiwa Tanzania.
Hata kama Feza akiamua kuhamia kabisa Botswana, hakuna tatizo kwakuwa atakuwa karibu na mchumba wake na hatokuwa mtu wa kwanza kumfuata mchumba wake kwao.
So kama kuna mtu atamuona Feza, amwambie asiwe na shaka, maisha ni popote.