Search in This Blog

VIOJA NA VITUKO VYA MISS TZ 2013

“Nimefurahi sana kwa sababu mshindi ana rangi ya asili kama Watanzania wengi tulivyo, lakini jamani namshauri asijaribu kutumia mkorogo, utamharibu vibaya jamani, naomba mumfikishie ushauri wangu,”
Miss Tanzania 2013, Happiness Watimanywa (katikati) akiwa katika pozi na mshindi wa pili, Latifa Mohamed (kulia) na mshindi wa tatu, Clara Bayo.
Shindano la kumsaka Miss Tanzania 2013, lililotimua vumbi usiku wa Jumamosi (Septemba 21, 2013), wiki iliyopita katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar lilitawaliwa na vituko vya hapa na pale, Ijumaa Wikienda lilikuwepo.
Katika shindano hilo, Happiness Watimanywa aliibuka Miss Tanzania 2013 na kuondoka na zawadi ya gari aina ya Toyota IST, akifuatiwa na Latifa Mohamed aliyeshika nafasi ya pili na Clara Bayo aliyeshika nafasi ya tatu.

Happiness Watimanywa akikabidhiwa ufunguo wa gari lake.
Ukianzia kwenye zulia jekundu (red carpet), baadhi ya walimbwende maarufu Bongo waligeuka vituko kwa kushindwa kupozi kwa ajili ya picha.
Pamoja na washiriki wote 30 kufunika kwa mavazi ya ubunifu, ufukweni na ya jioni, mtumbuizaji mkuu, Michael Ross kutoka Uganda hali ilikuwa ndivyo sivyo kwani wahudhuriaji wengi hawakuwa na mzuka wa shoo yake.
Baadhi ya warembo walichukua mataji mbalimbali yakiwemo Miss Photogenic lililoenda kwa Happiness Watimanywa, Miss Top Model, Narietha Boniface, Miss Talent, Prisca Clement, Miss Top Sports Woman, Clara Bayo na Miss Personality lililotua kwa Severine Lwinga.
Walioingia Top Five ya Miss Tanzania 2013 walikuwa ni Elizabert Perty, Clara Bayo, Lucy Tomeka, Latifa Mohamed na Happiness Watimanywa.

Lady Jaydee akitumbuiza.
Vituko vingine vilivyojitokeza ni pale washiriki hao wa Top Five walipokuwa wakiulizwa maswali ambapo mbali na ‘kimombo’ kibovu, mshiriki Elizabert Perty aliacha watu hoi alipoulizwa angetamani kukutana na mtu gani ambapo alisema kuwa angetamani kukutana na Mandela (Nelson) ambaye ni Rais wa South Africa ambaye alifungwa gerezani miaka 24.
Vituko katika maelezo yake ni kwamba aliomba kutumia lugha ya taifa lakini akaitaja Afrika Kusini kwa Kiingereza huku akisema Mandela ni Rais wa Afrika Kusini wakati alishastaafu na kwamba hakufungwa miaka 24 bali ni 27.
Huku akikosolewa kwa kushindwa kuwa na wacheza shoo lakini mwanamuziki Judith Wambura ‘Lady Jaydee’ alifanikiwa kuwainua mashabiki wake kwenye viti hasa alipoimba nyimbo zake za Joto Hasira na Yahaya huku mabuti yake yakigeuka gumzo.

Michael Ross akitoa burudani wakati wa shindano la Miss Tanzania 2013.
Katika shindano hilo ambalo baadhi ya warembo wa miaka ya nyuma walikuwa majaji wakiwemo Genevieve Mpangala, Faraja Kota, Jacqueline Ntuyabaliwe ‘K- Lynn’ na wengineo, mshindi aliwashangaza wengi kwani tofauti na miaka mitatu iliyopita ambapo walitoka Dar, mwaka huu imekuwa tofauti kwani Happiness anatoka Dodoma hivyo washiriki wa Dar waliangukia pua.
Baadhi ya wadau waliozungumza na Ijumaa Wikienda, walifurahishwa na mshindi kuwa na rangi ya kiasili (mweusi) na kumshauri kuitunza rangi yake hiyo na kuachana na matumizi ya ‘mkorogo’ ambao unaweza kuuharibu uzuri wake wa asili.
“Nimefurahi sana kwa sababu mshindi ana rangi ya asili kama Watanzania wengi tulivyo, lakini jamani namshauri asijaribu kutumia mkorogo, utamharibu vibaya jamani, naomba mumfikishie ushauri wangu,” alisema Emaculata Joel, mkazi wa Ubungo ambaye alikuwa miongoni mwa washiriki.


CREDIT GPL
 
Support : KARIBU TENA MDADISI MAM
Copyright © 2011. RISASI - Haki Zote Zimehifadhiwa.
KWA HISANI YA MDADISI MAMBO
Proudly powered by Blogger