MKE wa Rais Mama
Salma Kikwete amewataka wanafunzi wa kike kujiepusha na 'mafataki'
wanaotaka kuwarubuni kwa vitu mbalimbali ili kujikinga na hatari ya
kupata ujauzito na ugonjwa wa Ukimwi na kusababisha kutofikia malengo
katika maisha yao.
Pia amewataka wanafunzi wa kiume
kuachana na tabia ya kuvaa suruali milegezo na uvutaji wa sigara ambao
utawasababishia kupata ugonjwa wa saratani ya koo na mapafu.
Mama
Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo
(WAMA) alisema hayo hivi karibuni wakati akizungumza na wanafunzi wa
Shule ya Sekondari ya Msimbu iliyopo Kata ya Msimbu Wilaya ya Kisarawe
mkoani Pwani.
“Kama wazazi wenu hawawasimamii
kufuatilia mienendo yenu mjisimamie nyinyi wenyewe kwa kukanyana na
kutoa taarifa kwa walimu wenu pale ambapo mtaona mwenzenu ana tabia
ambazo ni kinyume na maadili ya mwanafunzi kwa kufanya hivyo mtaepukana
na tatizo la mimba za utotoni’, alisema Mama Kikwete.
Kuhusu madai ya wanafunzi hao kuwa
wazazi wao wanakabiliwa na tatizo la umasikini jambo ambalo linawafanya
waweze kuingia katika vishawishi mbalimbali Mama Kikwete alisema
umasikini isiwe ni kigezo cha mtu kufanya mambo yasiyofaa ili aweze
kupata fedha wakati ni hatari katika maisha yake.
“Ni muhimu wazazi wakatafuta mbinu
mbadala ya kuweza kukabiliana na hali hii ikiwa ni pamoja na kufanya
kazi kwani mtu akifanya kazi kwa bidii ni lazima atafanikiwa na kuweza
kupambana na hali ya umasikini kwani atalima mazao na kuuza, atafanya
biashara ndogondogo na kuweza kujipatia kipato”, alisema Mama Kikwete.
Aidha Mama Kikwete pia aliwataka
wanafunzi hao kuitumia teknolojia vizuri katika kujiletea maendeleo
ikiwa ni pamoja na kujitafutia nyaraka za kusoma kwa ajili ya masomo
yao.
Akisoma taarifa ya shule hiyo, Mwalimu
Mkuu Renatus Rweyemamu alisema tangu shule hiyo ilipoanzishwa mwaka 2007
hadi sasa idadi ya wasichana waliopata ujauzito ni 34 na wahusika
wameshafikishwa kwenye vyombo vya dola na hivi sasa suala hilo
linasimamiwa na watendaji wa vijiji husika.
Alitaja changamoto zinazoikabili shule
hiyo kuwa ni wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata shule jambo ambalo
linasababisha kuingia darasani wakiwa wamechoka.
Alisema pia wasichana wanakutana na
vishawishi vingi wakiwa njiani kutokana na hosteli moja haitoshi kwa
kuwa ina uwezo wa kuchukua wanafunzi 48 pia haina vitanda wala magodoro
ya kulalia.
Mwalimu Rweyemamu alisema, “Changamoto
nyingine ni wazazi kutofuatilia kwa ukaribu mienendo ya watoto wao pia
kutokutoa ushirikiano wakati wa kuwafuatilia wahusika waliowapatia
ujauzito watoto wao”.
Aliitaja mikakati waliyojiwekea kuwa ni
kufanya mikutano na wazazi ili kuwapa ushauri jinsi gani wanaweza
kufuatilia mienendo ya watoto wao na kutafuta wafadhili watakaowasaidia
kujenga hosteli ikiwa ni pamoja na kununua vitanda, magodoro na kuweka
umeme jua.
“Pamoja na majukumu mengi yanayokukabili ombi letu kubwa kwako kwa sasa ni tunaomba kama itawezekana utununulie vitanda na magodoro kwa hosteli yetu”, alisema Rweyemamu.
Shule ya Sekondari ya Msimbu ni shule ya
kata ambayo ina jumla ya wanafunzi 463 wasichana wakiwa ni 250 na
wavulana 213 ambao wanatoka katika vijiji sita vilivyopo katika Kata ya
Msimbu.