BABA AMUUA MWANAFUNZI WA SHULE YA MSINGI KISA MADAFTARI
OOAH! My God! Baba aliyejulikana kwa jina la Daniel Deogratus, mkazi wa Kitunda-Shule jijini Dar amekumbwa na tuhuma nzito akidaiwa kumuua kikatili mtoto wa kambo, Baraka Deo (9) kwa kipigo kikali huku akimuumiza vibaya mtoto wake wa kumzaa, Peter Masaka, wote madenti wa ‘primary’.
Tukio hilo lilijiri maeneo ya Kitunda, Dar, hivi karibuni ambapo mzazi huyo alidaiwa kuhusika na mauaji ya mtoto huyo na kumjeruhi mwanaye wa kumzaa kichwani kisa eti kikiwa ni madaftari tu.
Akizungumza kwa majonzi makubwa, mama mzazi wa marehemu, Veronica Jeremia aliliambia gazeti hili kuwa siku ya tukio mumewe huyo alirudi nyumbani saa 4:00 usiku akiwa amelewa ‘tilalila’ na kuwaambia watoto wake wamuoneshe madaftari ili aone kazi walizofanya shuleni siku hiyo.
Alisema kuwa watoto hao walimwambia baba yao kuwa hawakwenda shuleni kwani siku hiyo ilikuwa ni Jumamosi, akawaambia wamuoneshe kazi za jana yake (Ijumaa) hivyo watoto hao waliingia chumbani kwa ajili ya kuchukua madaftari wampelekee.
Alisema mumewe huyo aliamua kuwafuata watoto hao chumbani kwao huku akiwa na fimbo kisha akafunga mlango na kuanza kuwashughulikia.
“Niliposikia makelele ya watoto niliamua kwenda kugonga mlango,” alisema.
Alisema baada ya kugonga kwa muda mrefu bila mafanikio, mzazi mwenzake huyo alifungua na alipoingia, aliwakuta watoto hao wamelala kitandani wakiwa hawajiwezi huku marehemu akiwa amepasuka kichwani kwani alikuwa akiwapigiza ukutani, kuwagonganisha vichwa na kuwapiga kwa kutumia mbao.
Alisema baada ya kuona hivyo, alimwita mdogo wake kisha wakambeba mtoto Baraka hadi sebuleni akiwa hajitambui na kuamua kumkimbiza kwenye Hospitali ya Kitunda, Dar ambapo daktari aliwaambia wakachukue fomu ya matibabu polisi (PF-3) na baada ya hapo walimrudisha tena hospitalini hapo.
Alidai kwa muda wote huo, mtoto huyo alikuwa akitoka mapovu na damu mdomoni, masikioni na puani.
Mama huyo alisema kuwa wakati daktari akihangaika naye, mtoto huyo alikata roho.
Alisema baada ya kuona kaka yake amefariki, yule mtoto mwingine alianza kukimbia hovyo kutokana na maumivu ya kumuona mwenzake akiaga dunia.
“Ukweli ni kwamba daktari alijitahidi kujaribu kuokoa maisha ya mwanangu lakini ilishindikana kwani alikata roho nikiwa namuona. Nina maumivu makali sana moyoni mwangu, siwezi kusahau,” alisema mama huyo huku akilia kwa uchungu.
Habari zilieleza baada mauaji hayo, baba huyo alitaka kutoroka lakini wananchi wenye hasira walimkamata na kumfikisha katika kituo cha Polisi Sitaki-Shari kilichopo Ukonga-Segerea, Dar anakoshikiliwa akisubiri uchunguzi ukamilike ili sheria ichukue mkondo wake.