HUKUMU YA KODI YA LAINI YA SIMU NI LEO
Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, imesema itatoa uamuzi wake kesho dhidi ya pingamizi la awali la upande wa walalamikiwa la kuzuia kampuni za simu nchini kujiunga kwenye kesi ya kupinga tozo ya kadi ya simu ya Sh. 1,000 kwa kila laini na mtumiaji kwa kila mwezi.
Hatua hiyo ilifikiwa jana mahakamani hapo baada ya mabishano ya kisheria kati ya mawakili wa pande zote mbili huku mawakili wa Kampuni za simu za mkononi, Vodacom, Airtel, Mic Tanzania Ltd, TTCL na Zantel wakiomba mahakama ikubali kujiunga katika kesi ya msingi kati ya Chama cha Kutetea Walaji dhidi ya Mwanasheria Mkuu na Wizara ya Fedha.
Mabishano hayo yalitolewa mbele ya jopo la majaji watatu, wakiongozwa na Mwenyekiti Jaji Aloysius Mujulizi akisaidiana na Lawrence Kaduri na Salvatory Bongole.
Kabla ya uamuzi huo kutolewa, upande wa walalamikiwa ukiongozwa na Naibu Mwanasheria Mkuu, George Masaju, akisaidiana na Wakili wa Serikali Mkuu, Edson Mweyunge na Sara Mwaipopo, walipinga ombi la mawakili wa kampuni za simu la kutaka kujiunga kwenye kesi hiyo kwa kuwa hati ya kiapo ilikosewa kisheria.
Mweyunge alidai kuwa hati ya kiapo iliyowasilishwa mahakamani imeonyesha kutolewa na Tumaini Shija ambaye anawawakilisha walalamikiwa wengine zikiwamo zakampuni za simu.
“Sisi upande wa Jamhuri tunapinga mahakama kupokea kiapo hiki kwa sababu tayari mwombaji amekiuka taratibu za kisheria alitakiwa kuwasilisha maombi mahakamani ya kuwa mwakilishi wa wengine katika kesi hii ... hatuna uhakika kama TTCL imekubali kuwakilishwa na Shija kama kiapo kinavyoeleza kwa hiyo tunaomba mahakama itupe maombi hayo hayana mashiko ya kisheria,” alidai Mweyuge.
Alidai kuwa kwa sababu mwombaji ameruka hatua hiyo muhimu kisheria mahakama itupilie mbali maombi hayo.
Wakili wa kampuni za simu, Fatuma Karume, alidai kuwa pingamizi za Jamhuri halina sababu za msingi kwa sababu kiapo na kuwa siyo utaratibu wa kisheria kila mlalamikaji kuwasilisha hati yake ya kiapo katika kesi moja kwamba mahakama itupilie mbali pingamizi la Jamhuri halina msingi kisheria. Jaji Mjulizi alisema baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili mahakama itatoa uamuzi wa pingamizi la awali kesho na pamoja na maombi ya kesi ya msingi yatatajwa baada ya uamuzi huo.
Katika kesi ya msingi Chama cha Kutetea Walaji kimewaburuza mahakamani Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wizara ya Fedha kikitaka wapewe amri ya kusimamisha tozo ya kadi ya simu ya Sh. 1,000 kwa kila laini kwa watumiaji wa simu kila mwezi.