HAKIKA ni mateso, tena makubwa. Mtoto
Selemani Rajabu mwenye umri wa miaka 17, mkazi wa Ukonga kwa Guta,
jijini Dar yuko katika mateso makali baada ya mguu wake mmoja kuvimba
mithili ya tairi la gari kiasi kwamba hawezi kufanya jambo lolote zaidi
ya kujiburuza tu.
Akizungumza na gazeti hili nyumbani kwao
akiwa na simanzi kubwa, kijana huyo amesema kwamba anakumbuka amezaliwa
akiwa na ulemavu kidogo chini ya nyayo za miguu yake ambazo zilikuwa
nene kiasi cha kumfanya ashindwe kutembea na badala yake akawa ni mtu wa
kutambaa tu.
Alisema wakati huo alikuwa akiishi na
wazazi wake wote wawili, lakini baadaye wazazi hao walitengana na
kumfanya aishi na mama yake huko Pugu Kajiungeni. Kutokana na uwezo duni
wa mama yake, alimpeleka hospitali mara moja tu, licha ya mguu wake
kuendelea kuvimba kila siku.
“Nakumbuka mama yangu aliwahi kunipeleka
hospitali mara moja tu nilipokuwa mdogo, lakini sikumbuki kama aliwahi
kunipeleka tena,” alisema Selemani akiwa na sura ya kukata tamaa.
Alisema tangu wakati huo, mguu wake
uliendelea kuvimba siku hadi siku mpaka akashindwa hata kutambaa kama
mwanzo na sasa akalazimika kujiburuza licha ya uzito mkubwa wa mguu wake
kutokana na kuongezeka kwa uvimbe.
Kutokana na hali hiyo kuzidi kuwa mbaya,
alisema mwaka jana mama yake alimpeleka Hospitali ya CCBRT ambako baada
ya madaktari kumuangalia walisema mguu wake hauna maji ambayo wangeweza
kuyanyonya ili kuyatumia kupata vipimo na kujua tatizo linalomsumbua.
Hata hivyo, kwa bahati mbaya, mama yake
mzazi alifariki na kumlazimu baba yake kwenda kumchukua na kumpeleka kwa
bibi yake huko Manzese.
Hali ya bibi haikuwa nzuri kiafya, hivyo baba alinichukua tena na kuishi naye kwake nikiwa na mama wa kambo,” alisema Selemani.
Mtoto huyo analalamika kuwa anatamani
hata mguu wake huo ukatwe kutokana na adha anayoipata kwani anakosa raha
kama watoto wengine wanaotoka nje wenyewe tofauti na yeye anayetolewa
kwa kuburuzwa na watu zaidi ya wawili.
“Siku zote na raha kunapokucha najiona
kama sina thamani, natamani hata mguu huu ukatwe, siwezi kufanya kitu
chochote, natamani kuwa kama watoto wenzangu,” alisema.
Licha ya adha hiyo, Selemani alisema
kingine kinachomuumiza ni kufanya haja zote sehemu alipokaa na hivyo
kutoa wito kwa wasamaria, akiwemo Rais Jakaya Kikwete kumsaidia ili
aweze kupata matibabu.
Kwa wenye nia ya kumsaidia mtoto
Selamani, kwa matibabu au chakula, wanaombwa kuwasiliana na chumba cha
habari kwa simu namba 0713 612 533.