ALIYEKUWA KOCHA WA AZAM APATA SHAVU SUNDERLAND
ALIYEKUWA Kocha Mkuu wa timu ya Azam FC, Stewart Hall amepata ulaji mpya baada ya jana kujiunga na Klabu ya Sunderland AFC ya Uingereza akiwa Meneja wa ‘Kidongo Chekundu Sports Park’ pamoja na Kituo cha Michezo cha Elite Sports Academy vinavyojengwa Dar es Salaam.
Vituo vyote hivyo viwili vitakuwa chini ya Kampuni ya kufua umeme ya Symbion Power inayoshirikiana na klabu hiyo ya Ligi Kuu ya England, katika masuala mbalimbali ya ukuzaji wa vipaji vya michezo ambapo moja ya mikakati yake ni kujenga vituo mbalimbali vya michezo nchini kikiwamo cha Kidongo Chekundu.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana Dar es Salaam na Kitengo cha Mahusiano ya Umma cha Symbion Power, ikimnukuu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Symbion Tanzania, Peter Gathercole, ilisema Hall ambaye ni Mwingereza amesaini mkataba na kampuni hiyo bila kueleza ni wa muda gani.
“Stewart Hall, kocha wa soka Mwingereza, atajiunga na Symbion Power, kampuni kubwa ya kuzalisha umeme nchini, Sunderland AFC kutoka Uingereza, na Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, kama Meneja wa Kidongo Chekundu Sports Park pamoja na Elite Football Academy katika Jiji la Dar es Salaam,” ilisema taarifa ya Ofisa Mtendaji Mkuu huyo wa Sympion Power Tanzania.
Aidha, ilimnukuu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Sunderland AFC, Margaret Byrne akisema: “Tumefurahishwa kuona mradi wa kituo cha michezo unaokwenda kwa kasi. Uteuzi wa Stewart ni maendeleo ya kusisimua na tunajiandaa kuona juhudi kubwa kwa kila moja anayehusika ili kuleta matunda katika siku za usoni.”
Akizungumza jana Dar es Salaam, Hall alisema: “Mradi huu utaboresha haraka ubora wa wachezaji chipukizi katika ngazi ya klabu na timu za Taifa. Chipukizi watafundishwa masuala ya kiufundi, mbinu, kimwili na mahitaji ya kiakili katika soka ya kisasa. “Kutakuwa na programu iliyo sheheni ya ukocha. Nimefurahishwa kuhusu fursa ambazo zitaletwa kwa ajili ya Watanzania. Wachezaji bora watapewa fursa ya kunolewa katika Kituo cha Michezo cha Sunderland Academy of Light nchini Uingereza.”
Hall mwenye leseni ya ukocha ya Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) na kuwa Mkufunzi wa shirikisho hilo, alikuwa Kocha Mkuu wa Azam FC hadi kumalizika kwa mzunguko wa Ligi Kuu ya Bara, Novemba 7, mwaka huu walipoachana na klabu hiyo kwa makubaliano ya pamoja.
Amewahi kuifundisha timu ya soka ya Taifa ya Zanzibar, na pia ni aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Soka cha timu ya Birmingham City ya Uingereza.
Pia amewahi kufundisha soka akiwa Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Saint Vincent na Grenadines pamoja na Pune FC ya India na Sofapaka ya Kenya.
Baada ya kuachana na Azam FC, minong’ono ilienea katika duru za soka nchini kwamba anakwenda katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuwa Mkurugenzi wa Ufundi, jambo linalothibitika kuwa si kweli.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji wa Sympion Power Tanzania, Gathercole alisema mradi wa Kidongo Chekundu Sports Park, utakuwa wazi kwa watu wote ambao watakuwa wanacheza soka katika uwanja wenye nyasi bandia usiku pamoja na viwanja vidogo vitano, vya umri maalumu.
Kituo hicho kitakuwa na vyumba vya kubadilishia nguo, chumba cha madaktari chenye vifaa vya kisasa na mgahawa. Gathercole alisema ujenzi wake utaanza mwezi huu.
Hivi karibuni, Serikali kupitia kwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara ilitangaza kujengwa kwa kituo hicho, hatua iliyotokana na matunda ya ziara ya Rais Jakaya Kikwete na ujumbe wake katika kituo cha soka cha Sunderland, England, Juni mwaka huu.