MTIHANI wa Taifa wa Kidato cha Nne,
umeingia dosari baada ya walimu wawili akiwamo Mkuu wa Shule, kushikwa
wakishiriki kutoa majibu kwa wanafunzi wao. Tayari Polisi mkoani hapa,
inashikilia walimu hao wa Sekondari ya Nkinto wilayani Mkalama kwa
tuhuma ya kuvujisha mtihani huo unaoendelea kufanyika nchini kote hivi
sasa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida,
Geofrey Kamwela, alitaja watuhumiwa hao kuwa ni Mkuu wa Shule, Monica
Sebastian (30) na msimamizi wa mtihani huo, Agaloslo Otieno (32).
Alisema watuhumiwa hao walivujisha
mtihani huo juzi kati ya saa 3 na 3:30 asubuhi katika shule hiyo iliyopo
Kata ya Mwangeza Tarafa ya Kirumi.
Alidai kuwa Mwalimu Agaloslo aliyekuwa
akisimamia mtihani katika shule nyingine ya Mwangeza, aliandika baadhi
ya maswali ya Kiswahili na Uraia kwenye simu yake ya mkononi na kumtumia
Mkuu wa Shule yake ya Nkinto, Monica aliyekuwa shuleni kwake.
Baada ya Monica kupata maswali hayo,
inadaiwa alitafuta majibu akiwa chooni huku wanafunzi wakimfuata huko
huko na kupewa majibu.
Kamanda Kamwela alisema lengo lao
lilikuwa kusaidia wanafunzi, wafanye vizuri katika mtihani wao wa kidato
cha nne mwaka huu. Alisema wanafunzi waliishaambiwa wadanganye
wanakwenda chooni, ili wakapewe majibu na Mkuu wa Shule.
"Uchunguzi wa awali unaonesha kuwa
uvujishaji huo ulifanyika kwa nyakati tofauti kati ya Monica na Mwalimu
Agaloslo akiwa anasimamia mtihani huo katika shule tofauti.
“Baada ya Mkuu wa Shule kutumiwa
maswali, alijificha chooni na watahiniwa kwa nyakati tofauti waliomba
ruhusa kwa wasimamizi kwenda kujisaidia na hapo walimkuta Mkuu wa Shule
na kuwapa maelekezo ya namna ya kujibu maswali hayo," alisema Kamanda
Kamwela.
Alisema baada ya Polisi kupata taarifa
ya siri kutoka kwa wasamaria, iliweka mtego katika Sekondari ya Nkinto
na kumkamata Mwalimu Monica huku simu yake ikiwa na baadhi ya maswali ya
mtihani.