Search in This Blog

MWILI WA DR MVUNGI KUWASILI DAR LEO

MWILI wa aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi aliyefariki dunia Afrika Kusini, unatarajia kuwasili nchini leo. Taarifa ya awali kutoka NCCR Mageuzi alikokuwa Mkurugenzi wa Sheria, Katiba na Haki za Binadamu ilisema baada ya mwili huo kuwasili kwa ndege ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini utapelekwa katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo.
Kesho kutakuwa na ibada ya kumuaga itakayofanyika katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph na kisha kuagwa kwenye Viwanja vya Karimjee.
Baada ya Karimjee, mwili huo utapelekwa nyumbani kwake Kibamba Msakuzi ambako utalala na Jumapili itafanyika ibada nyumbani kabla ya kusafirishwa kwenda Kisangara Juu, Mwanga mkoani Kilimanjaro kwa maziko Jumatatu.
Shein amlilia Katika hatua nyingine, Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein amempelekea salamu za rambirambi Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba kutokana na kifo cha Dk Mvungi.
Katika salamu hizo, Dk Shein alieleza kusikitishwa na kifo hicho alichokielezea kuwa pigo kwa maendeleo ya Taifa na msiba wa Watanzania wote.
Dk Shein alimwelezea marehemu Mvungi kuwa mzalendo mwenye upendo mkubwa kwa nchi yake na mtaalamu wa sheria aliyebobea, mwanasiasa shupavu na makini. Aliongeza kuwa binafsi, wananchi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) wamehuzunishwa na kifo hicho.
Watuhumiwa bado Wakati huo huo, hatma ya watuhumiwa wa uvamizi wa Dk Mvungi ambao wanashikiliwa bado haijajulikana. Dk Mvungi alifariki dunia juzi alasiri katika Hospitali ya Milpark jijini Johannesburg Afrika Kusini alikokuwa akipatiwa matibabu baada ya kuvamiwa nyumbani kwake Kibamba, usiku wa Novemba 2. Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema jana kuwa:
“Nitafanya mkutano na waandishi wa habari ili kuzungumzia suala hilo ili umma uweze kujua ni watuhumiwa wangapi kwa ujumla na lini watafikishwa mahakamani.”
Hata hivyo, akizungumza na waandishi wa habari, Kova alisema hadi juzi watuhumiwa 10 walikuwa wamekamatwa wakihusishwa na tukio hilo.
Alisema Polisi inaendelea na msako dhidi ya wahusika wote ili wakamatwe na sheria ichukue mkondo wake.
 
Support : KARIBU TENA MDADISI MAM
Copyright © 2011. RISASI - Haki Zote Zimehifadhiwa.
KWA HISANI YA MDADISI MAMBO
Proudly powered by Blogger