MAWAZIRI watatu wa Serikali ya Rais
Jakaya Kikwete wapo katika wakati mgumu baada ya Katibu wa Itikadi na
Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Nape Nnauye, kutangaza rasmi kuwa
atahakikisha wanachukuliwa hatua za kuwajibishwa kutokana na kushindwa
kutekeleza majukumu yao.
Wakati Nape akitaka mawaziri hao
watimuliwe, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulhaman Kinana, amesema kuwa mawaziri
hao watawekwa kiti moto katika kikao kijacho cha Kamati
Kuu (CC), kwa lengo la kueleza ni hatua gani wanachukua katika
kushughulikia matatizo ya Watanzania.
Mawaziri hao ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Mhandisi
Christopher Chiza, Naibu wake, Adamu
Malima na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa
ambaye ametajwa kuwa sehemu ya matatizo katika kila wizara anayopewa
kuiongoza.
Akizungumza jana katika mkutano wa
hadhara uliofanyika katika Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Nape
alisema hakuna sababu ya kukaa kimya wakati mawaziri hao wameshindwa
kazi, hivyo ni vema wakawajibishwa ili kukiokoa chama chao.
Kuhusu Chiza na Malima, Nape alisema
mawaziri hao wameshindwa kutekeleza wajibu wao kwani tangu
walipochaguliwa kuongoza wizara hiyo hakuna hata siku moja ambayo
wamefika Ruvuma kushughulikia matatizo ya wakulima wakiwamo wa korosho,
tumbaku, mahindi na mpunga, ambapo katika mikoa mbalimbali nchini
imekuwa ikilalamikia sekta ya kilimo lakini wenyewe wamekaa kimya bila
kuchukua hatua zozote.
“Katibu Mkuu leo ni bora nikazungumza
haya ya mawaziri ambao wamepewa dhamana ya kuwatumikia Watanzania.
Nimeuliza hapa Ruvuma Waziri wa Kilimo na naibu wake walishawahi kufika
mara ngapi kushughulikia matatizo ya wakulima. Jibu lake, hakuna hata
siku moja wamefika.
“Hii inaleta tabu, wakati wakulima
wanahangaika na pembejeo za kilimo, ukosefu wa soko na malipo ya fedha
wanazodai serikalini mawaziri wenye dhamana wapo mjini wanafunga tai na
suti. Hawafikiri kuhusu matatizo ya wakulima,” alisema.
Aliongeza kuwa yupo tayari kupoteza
nafasi yake lakini hawezi kuvumilia hali hiyo ikaendelea na kutumia
nafasi hiyo kumuoma Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, ahakikishe
wanachukuliwa hatua na ikiwezekana waitwe CC wahojiwe.
Alisema karibu Tanzania yote wakulima
wamekuwa na matatizo mengi na wamekuwa wakilalamikia wizara hiyo na yeye
ni shahidi wa hayo yanayoendelea kutokea na ili kukinusuru chama hicho
mawaziri walioshindwa kazi wawajibishwe.
Alisema kuwa Wizara ya Kilimo, Chakula
na Ushirika imepewa dhamana ya kuwatumikia Watanzania asilimia 80,
ambayo ni wakulima lakini waliopewa jukumu hilo hawataki kufanya kazi
zao.
“Wananchi naomba mnilinde, lakini niseme
ukweli. Niseme nisiseme…mawaziri ambao tumewapeleka jikoni wameshindwa
kupika chakula, tunasubiri sebuleni lakini chakula hakiji.
Wanatukwamisha, ni bora wakaondoka kama wameshindwa kazi.
“Katibu Mkuu mimi nikija, sipo tayari
kuona CCM inakuwa chama cha upinzani bungeni kwa sababu tu ya hawa
wenzetu wachache ambao wanafanya makusudi na uzembe katika kutekeleza
wajibu wao,” alisema Nape.
Wakati kwa Dk. Kawambwa mbali ya
kushindwa kuongoza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi naye anatakiwa
kuchukuliwa hatua kutokana na mkataba aliouingia na makandarasi wa
ujenzi wa barabara ya kutoka Namtumbo hadi Tunduru mkoani Ruvuma.
Nape alisema anamshukuru Waziri wa
Ujenzi, Dk. John Magufuli, kwa kumfukuza mkandarasi huyo aliyemtaja kwa
jina la Progressive ambaye ameshindwa kazi ya kujenga barabara hiyo.
Hata hivyo, kumfukuza mkandarasi huyo
pekee haitoshi, hivyo aliyehusika kumpa mkataba anapaswa kuchukuliwa
hatua kwani uchunguzi unaonesha kuwa alishashindwa kazi na wakati
anapewa mkataba huo Waziri husika alikuwa Dk. Kawambwa.
“Dk. Kawambwa amekuwa akitukwamisha CCM
katika kutimiza wajibu wake. Hii barabara ya Namtumbo hadi Tunduru
kushindwa kukamilika imeleta aibu kubwa na kututia fedheha. Hivyo lazima
waliotoa mkataba wawajibishwe.
“Dk. Kawambwa huyu huyu ameshindwa
kushughulikia matatizo ya walimu nchini na atambue kuwa tulimpa muda wa
miezi sita na sisi tunahesabu, ukimalizika hatutaacha kuchukua hatua.
“Chama kitatumia wabunge wake kumuwajibisha. Hatuwezi kukaa kimya.
Iwapo ninaonekana kama kero kwa
kupigania masilahi ya nchi na watu wake, nipo tayari kuondoka na kwenda
kujihusisha na kilimo. Maana mimi ndiye mpiga debe wa chama, nitakwenda
kueleza nini kwa umma kutokana na ahadi zetu kukwama kwa sababu tu ya
uzembe wa wachache ndani ya serikali?” alihoji.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa CCM,
Kinana, alisema kuwa katika kikao kijacho cha Kamati Kuu (CC),
kitakachofanyika Desemba mwaka huu chama kitamuandikia barua Rais Jakaya
Kikwete ili mawaziri wake waje wajieleze mbele ya kikao kwa nini
wasifukuzwe kwa kushindwa kazi.
CREDIT: TANZANIA DAIMA