SAKATA la Mbunge wa Urambo Magharibi, Prof. Juma Kapuya (CCM) kudaiwa kumbaka mwanafunzi na kumtishia kumuua, linazidi kuchukua sura mpya ambapo Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema na Wizara ya Jamii, Jinsia na Watoto wamengilia kati.
Jana gazeti la Tanzania Dama liliripoti kauli ya Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu
ya Dar es Salaam, Suleiman Kova kuwa watamchukulia hatua Kapuya mara
moja baada ya mtoto huyo kuandikisha maelezo na kuwasilisha vielelezo
polisi.
Wakati hali ikiwa hivyo, huku chama chake, Chama Cha Mapinduzi (CCM)
nacho kikijinasua na kutaka Kapuya abebe mzigo wake mwenyewe, Tanzania
Daima limedokezwa kuwa IGP Mwema tayari ameingilia kati na kumwagiza
Kamishna Kova kuhakikisha suala hilo linashughulikiwa haraka.
Chanzo hicho kilidokeza kuwa IGP amelazimika kuingilia kati baada ya
kufuatwa na Naibu Waziri wa Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu,
aliyetaka kujua ni kwanini mtuhumiwa hachukuliwi hatua baada tuhuma hizo
kufichuliwa.
Taarifa za ndani zilidokeza kuwa serikali sasa inaendelea na
utaratibu wa kumwandalia Prof. Kapuya mashitaka ya ubakaji na kutishia
kumuua mwanafunzi huyo wa miaka 16.
Kwa siku tatu mfululizo Tanzania Daima limeripoti madai ya mtoto huyo
aliyedaiwa kubakwa na Prof. Kapuya, ambaye pia amewahi kushika nafasi za
uwaziri katika wizara mbalimbali.
Kwa mujibu wa ujumbe mfupi wa maandishi ya simu (sms) ambao Tanzania Daima linao, Prof. Kapuya kupitia namba iliyosajiliwa kwa jina lake
alitishia kumuua mtoto huyo na dada yake akitamba kuwa serikali hii ni
yao haiwezi kumfanya kitu.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Samuel Sitta, amesema nchi imefika pabaya kama viongozi wanaweza kutoa
vitisho na tambo za watoto wao kuuza dawa za kulevya, huku vyombo vya
dola vikishindwa kuchukua hatua.
Sitta ambaye pia ni spika mstaafu na Mbunge wa Urambo Mashariki,
alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki katika mahafali ya 15 ya kidato cha
nne ya Shule ya Sekondari Agape Seminari iliyoko Marangu, wilayani Moshi
vijijini.
Alisema kuwa nchi imegawanyika kimakundi, ambapo baadhi ya viongozi
wamekuwa na kiburi cha kutamba kwamba hawawajibiki kwa vyombo vya
kisheria.
Sitta alitolea mfano kitendo cha waziri mstaafu ambaye sasa ni
mbunge, aliyeripotiwa na vyombo vya habari akidaiwa kumtisha mtoto
aliyemtuhumu kuwa alimbaka mara mbili alipoitwa kwake kuchukua ada.
Katika moja ya ujumbe wa maandishi (sms), mbunge huyo ambaye Waziri
Sitta alimtolea mfano, anatamba na kumtisha binti huyo kuwa atamuua huku
akihoji: “Watato wetu wanauza unga nani anawakamata? Nani atapigana
nasi?”
Sitta alisisitiza kuwa Tanzania ni nchi kubwa, hivyo haiwezi
kuendeshwa hovyo hovyo, na kwamba lazima iendeshwe kwa viwango vya
maadili vitakavyoleta maendeleo.
-Tanzania Daima
-Tanzania Daima