Mwasisi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edwin Mtei
amesema kuwa chama hicho kitaendelea kuwafukuza wote wanaokihujumu huku
akieleza kwamba, anaunga mkono kuvuliwa uongozi kwa Zitto Kabwe na Dk
Kitila Mkumbo.
Akizungumza katika mahojiano maalumu , nyumbani kwake
jana, Mtei aliyewahi kuwa Gavana wa Benki Kuu (BOT) na Waziri wa Fedha
katika utawala wa awamu ya kwanza wa Mwalimu Julius Nyerere, aliweka
wazi kuwa daima ataunga mkono dhamira ya kukisimamia chama hicho
aliyoitaja kuwa ni safi.
“Naunga mkono uamuzi wote wa Kamati Kuu, kuwasimamisha na kuwavua
uongozi Naibu Katibu Mkuu wetu Zitto Kabwe na Dk Kitila Mkumbo. Na kwa
sababu Chadema inataka kusonga mbele, lazima iwafukuze mafisadi na wezi
wanaoshirikiana kukihujumu chama,” alisema Mtei.
Bila kufafanua zaidi au kutaja majina, mwenyekiti huyo wa kwanza wa
Chadema alisema: “Hatuwezi kuendesha chama wakati viongozi wengine
wanapokea pesa na kuzihifadhi kwenye akaunti za siri.” Alisisitiza
kwamba kwa nafasi yake akiwa mwasisi wa Chadema ni lazima ahakikishe
anaunga mkono dhamira safi ya kukisimamia chama.
Kuhusu Arfi kujiuzulu
Akizungumzia hatua ya Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), Saidi Arfi
kujiuzulu, Mtei alisema kuwa inafaa kiongozi huyo ajitazame upya na
kujisahihisha badala ya kuwa mlalamikaji kila siku.
“Aache kulalamika kwa sababu, wakati alipochaguliwa kuwa Makamu
Mwenyekiti mimi nilisimamia uchaguzi. Kama alikuwa na ndoto kwamba siku
moja atakuwa mwenyekiti wa Chadema taifa alipaswa kujichunguza kwanza,”
alisema.
Mtei aliongeza kuwa iwapo kuna watu wanadhani Chadema itakufa hiyo ni
dhana potovu, lakini kwa sasa chama hicho kimejipanga kuchukua dola na
tayari wamejiimarisha kimkakati.
“Katika suala la kushughulikia watu wanaokihujumu chama hakuna
‘compromise’ (mjadala),” alihitimisha Mtei. Juzi Chadema ilitangza
uamuzi wa Kamati Kuu yake kuwavua uongozi Zitto Kabwe na Dk Kitila, huku
Arfi akitangaza kujiuzulu nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Chadema
Tanzania Bara.
Mtei amewahi kumkemea na kumwonya Zitto katika mambo mbalimbali
aliyofanya ndani ya Chadema, moja ikiwa Oktoba mwaka jana ambapo mbunge
huyo wa Kigoma Kaskazini, alipotangaza kuwania urais mwaka 2015.
Alisema kuwa hatua hiyo itasababisha mzozo na mpasuko ndani ya chama,
huku akiongeza kwamba amekuwa akimshauri Zitto mara kwa mara kuhusu
hatua yake hiyo akimtaka kuwaunganisha wana-Chadema na siyo kuwagawa au
kuwavuruga.
“Hakuna shida kuonyesha hisia, lakini unatengeneza mzozo mkubwa sana
ukitangaza sasa. Mimi nimeshamshauri sana Zitto, ahakikishe
anakiunganisha chama na siyo kukigawa wala kukivuruga,” alisema Mtei.
Mtei alisema hatua ya mbunge huyo kutangaza kutogombea tena ubunge na
badala yake kujipanga kuwania urais mwaka 2015, imekuja mapema mno na
kuonya kuwa itaibua mzozo ndani ya Chadema, akiweka wazi kuwa wakati
ukifika chama hicho kitafanya uchaguzi sahihi.
“Siyo vibaya kwa Zitto kuonyesha hisia zake, lakini ndani ya Chadema kwa
sasa, kuna watu mbalimbali wanaopenda kuwania urais, lakini
hawajatangaza. Dk Slaa (Willbrod) anataka, Freeman (Mbowe) anataka,
Zitto anataka, hata mimi huenda nikataka kugombea. Hapa hakuna
upendeleo, sifa ndizo zitakazoamua,” alisema.
Hata hivyo, Zitto alipinga kauli hiyo akisema: “Demokrasia haileti
mizozo kwenye vyama vya siasa hata siku moja, bali humaliza mizozo.
Udikteta, kuminya fikra huru na mawazo huru, ndivyo huleta mizozo kwenye
vyama vya siasa.”
Alisema ni muhimu wazee wakawaacha vijana wawe huru kusema
wanachofikiri, kwa kuwa uhuru wa fikra na mawazo ni moja ya haki za
msingi na moja ya nguzo za demokrasia.
“Ninarudia, nitaomba kupeperusha bendera ya chama changu kwenye uchaguzi
wa urais mwaka 2015. Naamini kwamba ninaweza kuwezesha chama chetu
kushinda na kuongoza dola na Chadema kutoa rais wakati baadhi ya waasisi
wetu wakiwa hai na kuona vijana wao tunavyobadili maisha ya Watanzania
na kutimiza ndoto zao,” alisema Zitto.
Alisema ana uwezo, uadilifu na uzalendo wa kutosha kuwa Amiri Jeshi Mkuu
na kuunganisha Watanzania kuwa wamoja bila kujali rika, dini wala
makabila yao... “Nimejiandaa kisaikolojia kukabili changamoto za ufukara
wa nchi yetu.”