YANGA na Azam kama zinamtaka straika wa zamani wa Simba, Emmanuel Okwi ni fedha yao tu, lakini kuna sharti lazima walifanye.
Shirikisho la Soka Tanzania(TFF) limetoa
masharti na muongozo wa klabu zinazomtamani mchezaji huyo aliyesitisha
mkataba na Etoile du Sahel ya Tunisia.
Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, Saad
Kawemba aliiambia Mwanaspoti kuwa: “Hakuna kinachoizuia klabu kutaka
kumsajili Okwi, cha muhimu wanatakiwa kuongea na Etoile du Sahel ya
Tunisia, wakimalizana nao basi watamchukua, hivyo ni ruksa cha muhimu ni
kufuata sheria na haki.”
Okwi ameidhinishwa na Shirikisho la Soka
la Kimataifa (Fifa) kuichezea SC Villa ya Uganda kwa muda wa miezi sita
huku sakata lake la Etoile likifanyiwa ufumbuzi.
Mchezaji huyo anaidai Etoile malimbikizo
ya mishahara pamoja na dau lake la usajili huku Simba iliyomuuza kwa
Waarabu hao nayo ikidai dau lake Sh 480 milioni.
Suala hilo lipo Fifa na Kawemba amewahakikishia Simba kwamba wasiwe na wasiwasi watapata haki yao.