Wakati nyoka akiendelea kuwa adui mkubwa wa binadamu na konokono kuonekana mdudu anayetia kinyaa kwa baadhi ya watu, nchi za China na Japan wanyama hawa wamekuwa wakitumika kama mboga na wakati mwingine wamekuwa ni rafiki wa binadamu kwani wengi wao hufugwa na binadamu.
Lakini Ukistaajabu ya Musa utayaona ya Firauni,
kwani katika nchi za Ulaya miezi kadhaa iliyopita watu mbalimbali
wameanza kupokea tiba kutoka kwa wanyama hao ikiwemo huduma ya kukanda
na kupodoa uso (facial) inayotolewa na konokono na kusinga (massage)
inayotolewa na nyoka.
Facial ya konokono
Kwa wengi wetu konokono ni mdudu mpole zaidi
kuliko wadudu wengine wanaopatikana majanini, lakini nchini Japan
wataalamu wamegundua kuwa lami (uteute) anaotoa mdudu huyo ni tiba nzuri
kwa ngozi ya binadamu, baada ya kutumika kwa miezi kadhaa nchini Japan
sasa tiba hiyo imeanza kupendwa barani Ulaya, kama watu wanavyomiminika
katika saluni moja iliyopo East Midland nchini Uingereza.
Matibabu hayo yanahusisha konokono kuanzia watatu
ambao huwekwa juu ya uso wa binadamu na wao huanza kuzunguka maeneo
mbalimbali ya uso huo, yamekuwa yakiongeza uwingi wa watu katika saluni
za maeneo mbalimbali ya nchi za Ulaya.
Wataalamu hao wa facial ya konokono akiwamo Dk
Sunil Chopra wanasema kwamba katika matibabu hayo huwa wanahakikisha
kwamba konokono anatembelea kila sehemu ya uso wa binadamu isipokuwa
maeneo ya mdomo, macho na pua.
Kwa mujibu wa mmiliki wa Simply Divene Saloon
iliyopo Corby katika mji wa Northamptonshire nchini Uingereza, Diane
Gower matokeo ya tiba hiyo inayogharimu kiasi cha dola 50 sawa na
Sh80,000, huonekana papohapo na kwamba wadudu hao hutoa kamasi zenye
protini muhimu kwa ngozi ya binadamu.
Anasema, “Mwanzoni kwa mteja wa kwanza huwa
wanashtuka sana kwani anapokutembea usoni huona kuwepo kwa hali
isiyokuwa ya kawaida, lakini wateja wetu huhisi raha ya ajabu pindi
konokono wanapoendelea kutambaa kwenye nyuso zao kwa matibabu.”
Facial ya konokono ilianzishwa katika saluni
iitwayo Tokyo’s Clinical Saloon nchini Japan na mtu wa kwanza kupatiwa
huduma hiyo alikuwa ni mtu mmoja maarufu nchini humo, Escargot Course
mwanzoni mwa msimu huu na kulipia gharama ya dola 161 sawa na Sh
257,600.
Konokono 60 wanamilikiwa na Gower na wamekuwa wakipewa vyakula maalumu, ikiwemo matunda na mboga za majani.
“Hivi sasa watu wengi nchini Japan wanazalisha
konokono kwa ajili yetu na hata wengine wanazalisha kwa ajili ya chakula
kama utamaduni wetu ulivyo lakini wanatofautiana,” alisema Gower na
kuongeza; “Hii si aina ambayo unaweza ukaipata katika bustani, tumekuwa
tukiwaelekeza tunahitaji wa aina gani, hata hivyo tunawapa majina ya
aina ya konokono tunaowahitaji pia.”
Anasema wafanyakazi wote wa saluni wamepewa
mafunzo maalumu ya kushika konokono wanapomhudumia mteja, wengine
wanajifunzia katika saluni hiyo na baadaye wanakwenda kufanya kazi
sehemu nyingine tofauti.