NOOR SHIJA
Wanasayansi katika kurahisisha shughuli za binadamu wamevumbua
kifaa cha kutoa amri kwa masafa ya mbali kwa ajili ya mbwa (remote
control) na hasa kwa mbwa wanaotumika kwenye shughuli za uokoaji
yanapotokea majanga ya asili na wale wanaotumwa kusaka vitu haramu
vilivyofichwa kwenye maeneo yasiyofika kwa urahisi na binadamu.
Mbwa hutumiwa na binadamu kwa shughuli mbalimbali,
zikiwamo za kiaskari ambapo vyombo vya usalama hutumia mbwa kubaini
vitu vya hatari, uokoaji hasa panapotokea tetemeko la ardhi na watu
kufukiwa na kifusi, ulinzi na wengine humtumia kama rafiki kwa kuzurura
nao mitaani.
Kifaa hicho kilichowekwa mfumo wa GPS (Global
Positioning System) unaotumia mawasiliano ya satellite, huvikwa mgongoni
mwa mbwa na kumwezesha mmiliki wake kutoa amri akiwa masafa ya mbali.
Wanasayansi wa Chuo Kikuu cha Auburn kilichopo
Alabama, Marekani, wamefanya utafiti huo na kuvumbua kifaa hicho kwa
ajili ya kuwasaidia polisi wa kikosi cha mbwa kufanya kazi zao kwa
urahisi na bila kulazimika kuongozana na mbwa wao kila mahali.
Kifaa hicho kilichojengwa kwa kuwekwa GPS,
kinafungwa mgongoni mwa mbwa na kinaelekeza kwa kutoa ishara mbili
ambazo ni kutikisika na kutoa sauti, na zote hizo mbwa anakuwa
amefundishwa namna ya kuzitii.
Wanasayansi wametengeneza kifaa hiki hasa kwa
matumizi ya vyombo vya usalama, ambao mbwa kwao ni askari mwenza. Kwa
Marekani, GPS ilitengenezwa kwa madhumuni ya kijeshi, lakini kwa miaka
1980 ilianza kutumika kwa shughuli za kiraia.
Mbwa anapofungwa kifaa hicho ambacho kinatumia
mawimbi kama yale ya simu za mkononi au redio, hupokea amri kutoka kwa
bosi wake ambapo wanasayansi wamethibitisha kuwa utendaji kazi wa kifaa
hicho uko kwa asilimia 97.
Wanasayansi wamesema kifaa hicho licha ya
kuwasaidia wanausalama, pia kina uwezo wa kutumiwa na mtu mwenye mbwa
wake nyumbani, ambapo anaweza kumuachia akazurure mitaani na anaweza
kumwamuru arejee nyumbani wakati wowote anapotaka.
Kwa mujibu wa watafiti wa Chuo Kikuu cha Auburn,
kifaa hicho kinatoa sauti maalumu ambayo hufunzwa mbwa namna ya kuitii.
Kimetengenezwa maalumu kwa polisi wa kikosi cha mbwa, waongozaji na
kikosi cha uokoaji na kwa vitendo vyote hivyo usahihi wa utii ni
asilimia 97.
Wanasayansi Jeff Miller na David Bevly ambao ndiyo
wavumbuzi wa kifaa hicho, walikuwa na mawazo tangu mwanzo kusaidia
namna ya kuongoza mbwa kwa masafa marefu bila mmiliki kulazimika kuwa
jirani naye.
Kwa mujibu wa wanasayansi Miller na Bevly kifaa
hicho si cha kumwelekeza tu mbwa eneo la kwenda, pia kinatuma ujumbe
kumweleza muongoza mbwa kama kuna kitu kimegunduliwa.
Wanasayansi hao wanasema kina uwezo wa kupiga na kutuma picha na kumwezesha mmiliki kujua kilichogunduliwa na mbwa.