Beki kisiki wa kati wa Yanga, Kelvin Yondani.
Na Wilbert MolandiUONGOZI wa Klabu ya Simba umesema kuwa kama ukifanikiwa kumnasa beki kisiki wa kati wa Yanga, Kelvin Yondani, basi Gilbert Kaze raia wa Burundi ataondoka.
Inaelezwa kuwa tayari Simba imeanza mazungumzo ya kuhitaji kumrejesha mchezaji huyo licha ya kuwa amekuwa na nafasi ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga.
Taarifa kutoka ndani ya Simba ambazo zimefika kwenye dawati la gazeti hili, zimeeleza kuwa Kaze anaweza kuondolewa kwa kuwa aina ya uchezaji wake haina tofauti na Joseph Owino ambaye wamekuwa wakicheza pamoja naye, msimu huu.
Taarifa hizo zinaeleza kuwa benchi la ufundi hivi sasa linahitaji beki mwenye akili, kasi na nguvu ndani ya uwanja ili aendane na Owino na jina la Yondani ndilo ambalo limependekezwa.
“Simba wamedhamiria kuijenga upya timu yao kwa kuanzia kwenye usajili wa dirisha dogo la usajili msimu huu na katika usajili mkubwa wa msimu ujao,” kilisema chanzo cha uhakika.
Yondani aliondoka kwenye klabu hiyo baada ya maelewano mabaya kati yake na aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Moses Basena.
Alipoulizwa Mwenyekiti wa Usajili wa Yanga, Abdallah Bin Kleb alisema: “Tayari tumeanza mazungumzo na baadhi ya wachezaji tunaowahitaji kwa ajili ya kuwaongezea mikataba mipya ambao hatutawataja hadi tutakapomalizana nao.”