TUME ya Uchaguzi nchini (NEC) inadaiwa
kuingia katika mchakato wa mwisho wa kuzipa zabuni ya kuandaa vifaa vya
Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 kampuni za M/S Jazzmatrix Cooperation na M/S
Invu IT Solution zinazodaiwa kuwa na rekodi mbaya ya utendaji.
Tanzania Daima limedokezwa kuwa mkakati
huo unahusishwa na njama za kutaka kukibeba Chama Cha Mapinduzi (CCM)
katika uchaguzi huo kwa kuchakachua matokeo ya kukibakiza madarakani.
Kampuni hizo ambazo katika zabuni ya
Tume ya Uchaguzi zimetajwa kushirikiana na Kampuni ya Kitanzania ya M/S
SCI Tanzania Limited, mbali ya kutojulikana zinapotoka, pia ndizo
zimekuwa na gharama kubwa kuliko kampuni nyingine zilizoomba kazi hiyo.
Kiwango ambacho kampuni hizo zilitaja na
kukubaliwa na NEC kwa ajili ya kuandaa vifaa vya kielektroniki vya
kusajili wapiga kura (Biometric Voters Registration) ni zaidi ya euro
milioni 60, sawa na sh bilioni 126.3, wakati kampuni zinazofuata
zikihitaji kuanzia euro milioni 40.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zitto Kabwe, ni mmoja wa viongozi
waliofichua mkakati huo, akidai unafanywa na serikali ya CCM ili
kuhakikisha wanajiandaa kudhibiti kila eneo ili waweze kubaki
madarakani.
Alisema lengo ni kuhakikisha mchakato wa
vitambulisho vya kupigia kura vya kielektroniki vina kuwa na faida kwa
CCM na kukiingizia fedha chama hicho za kutumia kwenye uchaguzi huo
kupitia mfumo huo dhaifu wa vitambulisho hivyo.
Zitto alisema kutokana na hali hiyo,
amemwandikia Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) barua ya kutaka
ukaguzi wa zabuni hiyo ufanyike kwa kushirikisha Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru) na vyombo vingine vya usalama kwa ajili
ya kujiridhisha.
“Wenzetu CCM wanafanya mikakati ya
kujiandaa na Uchaguzi Mkuu wa 2015 kwa kuhakikisha wanapata fedha za
kutosha na hata mazingira mabaya ya vifaa vitakavyotumika katika upigaji
kura na sasa wameshaingia hata katika Tume ya Uchaguzi kwa ajili ya
kutengeneza mazingira,” alisema Zitto.
Aliongeza kuwa kiasi kilichotolewa ni
kodi ya Watanzania na kwamba ni vema taifa likajiridhisha kuwa matatizo
yaliyotokea Kenya na Ghana hayatajirudia Tanzania, hasa wakati wa
upigaji kura.
Gazeti hili limeona barua hiyo ya Zitto
kwenda kwa CAG, ya Novemba 7, 2013, yenye kichwa cha habari; ‘Zabuni ya
Biometric Voters Registration (BRV KITS) No. IE/018/2012-13/HQ/G/19
yenye thamani ya sh bilioni 126.3.’
Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini anasema kuwa NEC imekuwa katika mchakato wa zabuni tajwa hapo juu.
“Zabuni hiyo sasa imeanza kuleta
malalamiko miongoni mwa wananchi kutokana na kinachosemekana kuwa
kampuni iliyopewa zabuni hiyo haina uwezo kiteknolojia, pia bei zao ni
kubwa.
“Katika mafunzo ya hivi karibuni ya
SADCOPAC jijini Nairobi tuliazimia kuwa ni vema kwenye zabuni nyeti kama
za namna hii, SAIs wawe na uwezo wa kufanya ukaguzi kabla ya zabuni
kutolewa na kuanza kutekelezwa,” alisema.
Kwa mujibu wa nyaraka za NEC ambazo
Tanzania Daima linazo, kampuni zilizopewa tenda ya pamoja yenye
kugharimu kiasi cha dola 78, 987,636.00, sawa na sh 126,291,375,455 ni
M/S Jazzmatrix Cooperation na M/S Invu IT Solution ambazo hazijulikani
nchi zinapotoka zikiwa zinashirikiana na M/S SCI Tanzania Limited.
Katika nyaraka hizo kampuni zilizokosa
tenda na ambazo zimelalamika kwa Mkurugenzi wa NEC namna mchakato wa
kutoa zabuni hiyo ulivyoendeshwa zimeainishwa kuwa ni M/S Zetes SA ya
nchini Ubalgiji, M/S IRIS Corporation Technology ya Malaysia, M/S
Lithotech Exports ya Afrika Kusini, M/S Safran Morpho ya Ufaransa na
M/S Avante International Technology, Inc ya Marerkani.
Kampuni hizo zinahoji njia na sababu
zilizowafanya wakose tenda hiyo licha ya kuwa na uzoefu, vifaa bora
pamoja na kuwa na kiwango kidogo cha gharama tofauti na kampuni
iliyopewa kazi.
Katika moja ya malalamiko yao, Kampuni
ya M/S Morpho, inalalamika kutofahamishwa namna walivyokosa vigezo vya
kupata kazi hiyo licha ya kuwa na sifa za kimataifa za kufanya kazi huku
ikiwa imetoa bei nafuu kuliko kampuni iliyopata kazi.
“Tulikuwa miongoni mwa washindani
muhimu kwa kuwa kiwango chetu kilikuwa ni sh bilioni 97.8 ambazo ni sawa
na euro 44,939,912 + sh 3,843,736,140.
“Ujuzi, vigezo na uzoefu wetu
havilingani, duniani kote tumefanya kazi katika maeneo mengine kwa
ufanisi na tunashindwa kuelewa kivipi walishinda hao ambao wamepata kazi
kwa kiwango cha zaidi ya sh bilioni 27.8 ikilinganishwa na yetu,”
ilisomeka sehemu ya barua.
Alipotafutwa Mkurugenzi wa NEC, Julius
Mallaba, alisema hawezi kuliongelea suala hilo katika simu na kuomba
mwandishi awasiliane na Kaimu Mkurugenzi wa NEC, Dk. Sist Cariah, ambaye
alisema mchakato wa kupata kampuni ulifuatwa kisheria.
Dk. Cariah alisema si kweli kwamba
kampuni iliyopewa kazi haina uwezo bali malalamiko yanatoka kwa watu
walioshindwa kupata kazi hiyo.
Alipoulizwa juu ya uzoefu wa kampuni
hiyo na wapi ilifanya kazi, Dk. Cariah alisema kwa maelezo waliyonayo ni
kwamba kampuni hiyo ina uzoefu wa miaka 35 wa kufanya kazi, huku
akishindwa kuainisha sehemu ilizowahi kufanya kazi.
Kuhusu wapi zimetoka kampuni hizo, Dk.
Cariah alisema suala la kutoainishwa kimaandishi ni makosa ya kawaida,
huku akitaja kuwa zinatoka katika nchi ya India na Australia.
Kuhusu gharama, Dk. Cariah alisema licha
ya makampuni mengine kutaja gharama za chini, zingeweza kuwa na gharama
kubwa zaidi wakati wa kukamilisha kazi hiyo kutokana na kuwa na gharama
zilizojificha.
Chanzo :Tanzania Daima