Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi Mkuu
wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Upasuaji wa Mishipa ya Fahamu Muhimbili
(Moi), Profesa Lawrence Museru alisema anachofahamu ni kuwa Dk Mvungi
alipelekwa Afrika Kusini kwa kuwa alipata madhara makubwa kwenye ubongo
na wala si kwa sababu ya kumwagika kwa maji kama ilivyoelezwa Afrika
Kusini.
Hospitali ya Millpark ya Johannesburg,
Afrika Kusini, imesema madaktari waliokuwa wakimtibu aliyekuwa Kamishna
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi walibaini kuharibika
kwa ubongo wake kutokana na kumwagika kwa maji yanayoutunza ambayo
kitaalamu yanaitwa ‘cerebrospinal fluids’ au CCF.
Msemaji wa Hospitali hiyo, Tebogo
Nyembezi alisema Dk Mvungi alicheleweshewa tiba baada ya kupata tatizo
la maji hayo yanayotunza ubongo kumwagika mara baada ya kujeruhiwa.
Dk Mvungi (61), alipata majeraha makubwa
baada ya kujeruhiwa na watu waliovamia nyumbani kwake Kibamba, Wilaya
ya Kinondoni, Dar es Salaam, Novemba 3 mwaka huu. Alifariki dunia jana
mchana.
“Maji hayo ambayo ni miligramu 50 tu
katika ubongo wa mwanadamu ambayo huufanya ubongo uelee yakimwagika nusu
tu, basi mgonjwa yupo hatarini, lakini akiwahishwa na kupata tiba
sahihi anaweza kupona,” alisema Nyembezi.
Alisema iwapo mgonjwa atapewa tiba
sahihi ndani ya saa 48, ubongo wake unaweza kurudi katika hali ya
kawaida, lakini saa hizo zikizidi hawezi kupona kabisa kwa sababu maji
hayo yanapomwagika ubongo hujigonga kwenye mifupa ya sakafu yake na
kuharibika kabisa.
Mtaalamu wa mishipa na neva za fahamu
(neurosurgeon) katika Hospitali ya Regency, Dar es Salaam, Dk Hariff
Najin alisema kazi kubwa ya maji hayo ni kuulinda ubongo pindi
inapotokea ajali ili usidhurike lakini endapo maji hayo yatamwagika nao
huharibika.
“Haya maji yanaufanya ubongo uelee na
usielemee kichwa. Hivyo inapotokea maji haya yakaisha au kupungua,
ubongo hujigonga na kukosa ukinzani na kuharibika,” alisema.
Alisema maji hayo ambayo hufika hadi
kwenye uti wa mgongo yakikosekana katika ubongo, husababisha damu
isitembee kwenye eneo hilo jambo ambalo pia linaweza kusababisha mishipa
katika sehemu ya nyuma ya ubongo kuharibiwa.
Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi Mkuu
wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Upasuaji wa Mishipa ya Fahamu Muhimbili
(Moi), Profesa Lawrence Museru alisema anachofahamu ni kuwa Dk Mvungi
alipelekwa Afrika Kusini kwa kuwa alipata madhara makubwa kwenye ubongo
na wala si kwa sababu ya kumwagika kwa maji kama ilivyoelezwa Afrika
Kusini.
“Majeraha hayo yalisababisha damu
kuvilia katika ubongo na kusababisha uvimbe ambao kwa kitaalamu unaitwa
‘traumatic brain injury’ na sisi tulithibitisha vipimo hivyo vya awali
na kumsindikiza mpaka huko,” alisema Profesa Maseru.
Profesa Museru alisema Dk Mvungi alipata
majeraha makubwa kichwani na sehemu nyingine mwilini ambayo yanaonekana
yalisababishwa na kupigwa kwa vitu vyenye ncha kali au magongo na hivyo
kuleta madhara katika ubongo.
Alisema hawezi kuthibitisha chanzo hasa
cha kifo hicho kwani kinaweza kuwa ni kuharibika kwa ubongo au sababu
nyingine zilizotokana na tatizo hilo (secondary causes).
Naye Dk Mugisha Clement ambaye
alimuhudumia Dk Mvungi alipofikishwa Moi na baadaye kumsindikiza hadi
Afrika Kusini, alisema kitaalamu kumwagika kwa maji yanayolinda ubongo
hakuwezi kuleta madhara kama aliyoyapata mwanasheria huyo, bali tatizo
lilikuwa ni kuvimba na kuvilia damu katika ubongo.
“Maji ya CSF hayakuwa sababu ya kifo cha
Dk Mvungi, sisi tulitambua tatizo la awali kuwa majeraha yalisababisha
kuvimba na kuvilia damu. Kitaalamu haiwezekani maji hayo yakasababisha
madhara makubwa,” alisema.
Kucheleweshwa kwa matibabu
Kuhusu kutokuwapo kwa opereta wa mashine
ya CT Scan inayotumika kupima ubongo siku ambayo Dk Mvungi alipelekwa
Moi, Profesa Museru alisema hatua za kinidhamu zitachukuliwa.
Hata hivyo, alisema kukosekana kwake hakukusababisha au kuchochea madhara kwa Dk Mvungi.
“Ni kweli kutokuwapo kwa opereta ni kosa
lakini halikuwa na madhara kwa Dk Mvungi kwa sababu hakuwa akihitaji
upasuaji wa haraka. Lakini ni kosa limefanyika,” alisema Profesa Maseru.
Alisema matumizi ya CT Scan ni ya muhimu
lakini, hata kipindi cha nyuma ambacho wagonjwa walipata matatizo
katika ubongo bado walitibiwa bila ya kuwapo ulazima wa kupata huduma ya
mashine hiyo.
Source-Mwananchi