Stori: Makongoro Oging’ na Haruni Sanchawa
MKESHA
wa Mwaka Mpya (2014) ulikuwa ni kilio, huzuni na majonzi kwa wakazi wa
Pugu Kwamustafa, Ilala jijini Dar es Salaam kufuatia Meja wa Jeshi la
Wananchi Tanzania (JWTZ), Rashid Musa (43) kudaiwa kuwaua kwa kuwapiga
risasi hadi kufa madenti wawili na wengine watatu kujeruhiwa wakati
wakisherehekea mwaka.
Madenti waliouawa ni Ibrahim Mohamed (16), wa kidato cha tatu na
Abubakar Hassan (14), wa kidato cha kwanza Shule ya Sekondari ya
Kinyamwezi.
Kwa mujibu wa mashuhuda, siku ya tukio, Meja Rashid wa
Kikosi cha Jeshi Land Force Kibaha, alidaiwa kuwamiminia risasi vijana
hao waliokuwa wakishangilia kuuona mwaka mpya wakati walipokuwa wakivuka
barabara.
SHUHUDA NZITO
Kufuatia tukio hilo la
kuhuzunisha, mwishoni mwa wiki iliyopita, Uwazi liliwatafuta mashuhuda
wa tukio hilo na kuzungumza nao wanachokijua.
“Kwa jina naitwa Rashid Juma nina miaka kumi na tatu, nakumbuka siku
hiyo tulikuwa watoto wa kike na wa kiume, wengi wenye umri kati ya
miaka nane hadi kumi na saba, tulikuwa kama themanini hivi, ilipofika
saa sita kamili usiku tuliingia mitaani kushangilia kwa kuuona mwaka
mpya.
“Si mara ya kwanza sisi watoto wa mtaa huu kusherehekea mwaka mpya,
kila mara tunafanyaga hivyo na kurudi majumbani salama, lakini nashangaa
safari hii kipindi hiki hili balaa limetoka wapi?
“Ilipofika saa sita na dakika tano tukiwa tunaendelea kusherehekea
huku tukivuka barabara, tulipishana na gari la mwanajeshi huyo,
hatukumtukana wala, ghafla tulisikia mlio wa risasi, paa! Paa! Papapa!
“Kabla
hatujakaa sawa tulimwona mwenzetu (Abubakar) yupo chini huku akilia kwa
uchungu akihitaji msaada, kabla hatujakaa sawa tena risasi ziliendelea
kusikika, wengine wakiwa wamedondoka chini.
Mimi na wenzangu wengine tulikimbia, tulijua ni majambazi,” alisema shuhuda huyo, akaendelea:
“Baada
ya kutawanyika, tuliliona gari likiondoka katika eneo la tukio,
tukapiga kelele, ndipo wazazi wetu wakatoka nje na kuliona lile gari.
Wengine walilitambua kwa vile yule mwanajeshi anaishi karibu na maeneo
haya, amekuwa akipita na gari lake hilo mara kwa mara.
“Hata hivyo, yule mwanajeshi hakusimama, nasikia alikwenda hadi
kwake, tulirudi na kuwaangalia waliopigwa risasi ndipo tuligundua kuwa
wenzetu wawili walikufa na wengine walijeruhiwa.
MAJERUHI AZUNGUMZA
Naye mmoja wa majeruhi
aliyejitambulisha kwa jina la Agustina Pius alipohojiwa na Uwazi alisema
siku ya tukio alikuwa nje ya nyumba yake akiongea kwa simu na ndugu
zake wa mikoani akiwapongeza kwa kuuona mwaka mpya.
“Ghafla nikasikia milio ya risasi barabarani huku watoto waliokuwa
wakisherehekea wakipiga kelele za kusema tunakufa…tunakufa,” alisema
majeruhi huyo.
Aliendelea kusema kwamba kufuatia hali hiyo, aliweka
simu kwenye mfuko wa suruali na kuingia ndani, lakini ghafla alisikia
kitu kimepiga simu yake na kulipuka.
Aliitoa mfukoni ikiwa inawaka moto na kuitupa chini, alipojikagua
ndipo aligundua anatokwa na damu nyingi kwenye paja, alipoangalia chini
aliona risasi.
“Niliwaambia watu wa jirani yangu ambapo walinikimbiza Hospitali ya Amana kwa matibabu,” alisema.
BABA MZAZI WA MAREHEMU
Naye baba mzazi wa
marehemu Abubakar, mzee Hassan alipohojiwa kuhusiana na tukio hilo
alisema ni tukio la ajabu sana kwake kwani watoto hao kila mwaka katika
kuukaribisha mwaka mpya hutoka nje kuushangilia, anashangaa kusikia
wameuawa kwa risasi.
KAMANDA MINANGI
Jumamosi iliyopita, Uwazi
lilimfuata Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Ilala, Afande Marietha Minangi
Komba na kumuuliza kuhusu tukio hilo ambapo alikiri kulipokea, akasema:
“Uchunguzi wa awali unaonesha kwamba meja huyo alifyatua risasi
hewani kwa kudhani kuwa wale vijana walikuwa wahalifu, hivyo alikuwa
akijihami.
“Kwa sasa tunamshikilia (meja). Wakati wa kukamatwa kwake bastola
yake ilikuwa na risasi kumi, tano zilitumika katika eneo la tukio. Jeshi
langu linaendelea na uchunguzi na sheria itachukua mkondo wake,”
alisema kamanda huyo.
WALIOJERUHIWA
Waliojeruhiwa katika sakata hilo ni Lugano Wanga
(17), Kasim Abdul (16) na Agustina Pius (28) ambao walikimbizwa katika
Hospitali ya Amana kwa matibabu na kuruhusiwa.