KIJANA Haruni Kayombo (19), mkazi wa Mbalizi, Mbeya anaishi kwa
mateso makubwa tangu mwaka 2006, baada kushikwa na ugonjwa wa ajabu
uliomuanza ghafla.
Katika mahojiano na gazeti hili akiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili
(MNH) jijini Dar es Salaam, Kayombo alisema bado hajui hatima ya maisha
yake kutokana na mateso anayoyapata usiku na mchana huku akitoa simulizi
ya majonzi namna gonjwa hilo lilivyomtokea.
Alisema awali akiwa na umri wa miaka 11 alilazwa Hospitali ya Rufaa
ya Mbeya lakini baadaye wazazi wake walifariki dunia na hakupata kuwajua
ndugu zake jambo ambalo anaona hakuna haja ya kuwa binadamu huku
akionekana mwenye mateso makubwa.
“Sioni faida ya kuwa binadamu, niliugua kama utani, ilifika wakati
nikajua kitu cha kawaida, nilishangaa kuona linazidi kuongezeka nilijua
utakuwa ugonjwa wa muda mfupi, lakini nikashangaa usiku na mchana
mateso yanazidi.
“Ni tatizo ambalo hata mimi mwenyewe sijui chanzo chake, lilianza
kama kauvimbe ka kawaida, sikutambua mapema na sikuwa na hela kwenda
kwenye kituo cha afya kwa matibabu zaidi.
“Nilijipa moyo kuwa ipo siku nitakuwa sawa lakini kwa mpaka sasa
nimeshakata tamaa, sina baba wala mama, hapa kweli kuna haja ya mimi
kuitwa binadamu? Sina kazi na sikubahatika kusoma ni nani atakayeokoa
maisha yangu?
“Maisha haya ni Mungu tu anayeweza kuniokoa, inaniuma sana! Ningekuwa
na ndugu wangeweza kunisaidia japo hata pesa ya matumizi. Eee... Mola
okoa maisha yangu (analia). Napenda kuishi kama binadamu wengine lakini
kwa hali hii sina amani kabisa.
“Zamani wakati tatizo linaanza nilikuwa na tabia ya kusali mara kwa
mara lakini nimefika hatua ya kukata tamaa na kuona hakuna haja.
“Namuomba
rais aje anitembelee ajionee mateso ninayoyapata usiku na mchana,
nimepangiwa kwenda kufanyiwa operesheni India lakini sijui lini na
itakuwaje!” alisimua Kayombo na kumaliza na kilio tena.
Kama utakuwa umeguswa na tatizo la Haruni Kayombo basi usisite kutoa
mchango wako kwenye namba yake ya simu, mtumie kwa njia ya M-PESA ama
wasiliana naye moja kwa moja akiwa ndani ya Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili kwa namba +255764548607.