IKIWA ni takribani mwaka mmoja tangu alipoondokewa na mumewe,
marehemu Juma Kilowoko ‘Sajuki’, staa wa filamu Bongo, Wastara Juma
amesema sasa yupo tayari kuolewa lakini sharti la kwanza la muoaji
lazima awe mtu mwenye fedha zake.
Akizungumza na Risasi Mchanganyiko, wikiendi iliyopita jijini Dar es
Salaam, Wastara alisema, amekuwa mpweke kwa muda mrefu na sasa ni wakati
muafaka wa kumpata mtu wa kuziba pengo la marehemu mume wake.
“Inatosha
sasa, nadhani muda wa kuwa na mwenzangu umefika. Napenda huyo mwanaume
awe mwenye huruma, upendo na kutambua thamani ya mke lakini ni vizuri
akiwa mwenye kujituma na awe na fedha nyingi.
“Natamani kuolewa na bilionea. Najua nikiwa na mwanaume wa aina hiyo
sitateseka, nitapata kila ninachokitaka. Unajua mimi kama mwanamke nina
mambo mengi. Siyo siri natamani itokee siku moja niendeshe Hummer au
Prado (aina za magari) kulingana na hadhi yangu.
“Kiukweli
nitafurahi sana nikimpata mwanaume wa aina hiyo, maana nitakuwa na
uhakika wa kufanya mambo mengi ikiwa ni pamoja na kunisaidia katika
shughuli zangu za sanaa,” alisema Wastara.