HUKUMU iliyosomwa na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, John Utumwa, Jumanne iliyopita (juzi), imemuongezea uzito Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, sasa amekuwa mzito zaidi ndani ya chama chake.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe akiwa ndani ya Mahakama Kuu wakati akisubiri hukumu ya kesi yake juzi.
Awali, ilionekana kama uamuzi wa Kamati Kuu (CC) ya Chadema ni
msumari wa mwisho na kwamba Zitto hana uzito wowote wa kuutilia
changamoto lakini kile kilichoamuliwa na mahakama ni wazi kimemuongezea
nguvu mbunge huyo.
Wafuasi wa Zitto wakiwa na mabango wakati wa hukumu yake.
Hukumu ya Jaji Utumwa, ilimpa ushindi Zitto kuhusu pingamizi lake
aliloweka mahakamani akitaka mahakama iweke zuio kwa CC ya chama chake
kujadili uanachama wake mpaka atakapopewa fursa kukata rufaa katika
Baraza Kuu la Chadema.Kutokana na hukumu hiyo, baadhi ya wananchi walitoa maoni yao kwamba, Zitto anaweza kupumua sasa angalau kwa kiasi fulani kuweza kuuthibitishia umma kuwa, CC ilimuonea.
“Angeshindwa mahakamani, angekuwa na hatima mbaya kwenye chama chake, tena angefukuzwa uanachama mara moja lakini mahakama imempa nguvu, sasa uzito wake ni mkubwa na hata wanaomuunga mkono wanaweza kutembea kifua mbele,” alisema Shadrack Lyimo aliyekuwa mahakamani juzi.
Zitto, amefungua mashtaka mahakamani akimshitaki katibu mkuu wa chama chake na baraza la wadhamini kwa kutompa fursa ya kuukatia rufaa uamuzi wa CC wa kumvua nyadhifa zake zote na sasa kesi ya msingi itasomwa kwa mara ya kwanza Februari 13, mwaka huu.
Katika madai ya msingi, Zitto anataka katibu mkuu na baraza la wadhamini wa Chadema kumpa fursa ya kukata rufaa Baraza Kuu kwa maelezo kwamba, CC ilikiuka taratibu ya kumvua nyadhifa zote za uongozi.
Jaji Utumwa akisoma hukumu yake alisema CC hairuhusiwi kujadili uanachama wa Zitto mpaka hukumu ya kesi ya msingi itakapotolewa au pale Baraza Kuu litakapoitishwa na kusikiliza rufaa ya mbunge huyo.