Oooh! Nooh! Wakati akimpa mama yake, Sanura Kassim ‘Sandra’ gari la
Sh. milioni 38 huku akitawanya mamilioni ya fedha kwenye matukio
mbalimbali, staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’
anadaiwa kunyemelewa na laana kufuatia baba yake, Abdul Jumaa kuugua na
kuvimba miguu bila msaada wowote.
Kwa mujibu wa chanzo makini cha Ijumaa, baba wa staa huyo anayeishi
Magomeni-Kagera jijini Dar, amekuwa akisumbuliwa na tatizo la kuvimba
miguu na hakuna msaada wowote anaoupata kwani chanzo cha mapato
anachokitegemea ni kodi tu ya nyumba ambayo anaipata kutoka kwa
wapangaji wachache alionao.
BOFYA HAPA KUKISIKIA CHANZO
“Yaani tunashangaa
kusikia Diamond ana fedha nyingi, juzikati tuliona katika gazeti
kamnunulia mama yake gari la milioni 38 (Toyota Lexus-Harrier) sasa kwa
nini asimthamini baba yake hata kidogo?
“Ukweli ni kwamba baba Diamond anasumbuliwa na tatizo la miguu kuvimba.
“Amekuwa akilalamika mara kwa mara lakini Diamond hatujawahi
kumuona,” kilinyetisha chanzo hicho na kuongeza:“Juzikati hapa baba
Diamond alishikika kwelikweli miguu, akaugulia mwenyewe ndani pasipo
kuwa na msaada wowote tena nasikia mzee huyo hataki hata kuongelea
lolote kuhusu Diamond maana haoni umuhimu wa kufanya hivyo wakati
amemsusa muda mrefu sana.”
MATIBABU HAYAZIDI MILIONI
Katika aya nyingine,
chanzo hicho kilidai kwamba ugonjwa wa miguu ambao unamsumbua mzazi
huyo, gharama za matibabu haziwezi kufikia hata shilingi milioni moja za
madafu achilia mbali mamilioni anayoyatapanya staa huyo.
“Ingekuwa tatizo kubwa sana, hapo sawa, kwa sababu miguu huwa
inamvimba lakini akipata dawa za kutumia huwa inarudi katika hali ya
kawaida, kwa nini lakini anamfanyia hivyo baba yake? Amemkosea nini?”
Kilihoji chanzo hicho.
UTAJIRI WAKE WAANIKWA
Wakati chanzo hicho
kikiweka nukta hapo kwa muda, mapaparazi wetu walipewa malalamiko
mengine kutoka kwa jirani mmoja wa baba Diamond ambaye alimsihi amsaidie
mzazi wake kwani anaamini uwezo anao kupitia kumbukumbu ambazo Diamond
mwenyewe alizithibitisha kupitia vipindi mbalimbali vya runingani kama
Take One na Spora Show vya CloudsTV.
Pia kwenye vyombo vingine vya habari zikiwemo redio na magazeti pendwa ya Global Publishers.
Jirani huyo alidai kwamba mwaka jana Diamond alitangaza kuwa ana
utajiri wa Sh. bilioni moja ikiaminika kwamba mwaka huu umeongezeka mara
dufu.
“Nakumbuka mwaka jana kupitia Kipindi cha Spora Show na kile cha Take
One, Diamond alikiri kuwa ana mkwanja usiopungua bilioni moja, hiyo
ilikuwa kwa mwaka jana, sasa mwaka huu unadhani atakuwa na shilingi
ngapi? Aache hizo bwana, amsaidie baba yake hata kwa kumpa mtaji mdogo
wa biashara ambao unaweza kumsaidia,” alisema jirani huyo.
MATANUZI YA DIAMOND, WEMA
Katika kuendelea
kuichimba habari hiyo, mapaparazi wetu walinasa malalamiko kutoka kwa
jirani mwingine wa mzazi huyo ambaye alieleza masikitiko yake kwa
kulinganisha starehe ambazo staa huyo anazifanya na asali wake wa moyo,
Beautiful Onyinye, Wema Isaac Sepetu na maisha halisi ya baba yake.
“Mimi ni mfuatiliaji mzuri wa habari za mastaa, naona kila siku
kwenye vyombo vya habari jinsi gani Wema na Diamond wanavyotumia fedha
nyingi katika masuala ambayo hayana ulazima kiivyo.
“Sisi kama
majirani hatupendezwi na hali hii, angekuwa anakuja angalau siku
mojamoja kumuona baba yake kuliko kila siku kumhudumia mama yake pekee,”
alisema jirani huyo.
TATIZO NI NINI?
Mapaparazi wetu waliingia
mzigoni kusaka kiini halisi kwa nini Diamond amwage fedha nyingi kwa
mama yake pasipo kumkumbuka japo kiduchu baba yake ambapo ilielezwa kuwa
staa huyo wa Mdogomdogo hakuwa na ugomvi wowote na mzazi wake huyo.
“Kama ni ugomvi ulikuwepo kati ya mama na baba lakini Diamond
hahusiki, tunashangaa kuona kama staa huyo naye anaweza kumsusia baba
yake,” kilieleza chanzo na kuongeza:
“Mbaya zaidi nasikia Diamond amekuwa mzito kupokea simu za baba yake,
sasa huoni kama siyo jambo la busara, mzazi ni mzazi tu hata iweje. Kwa
mtazamo wangu kinachofuata ni laana.
“Kuna mifano ya watu wengi ambao waliingia kwenye laana za wazazi wao
na wakajikuta kama siyo kufulia kama (wanatajwa mastaa waliofulia wa
muziki Bongo) au hata kukutwa na umauti.
“Jambo hili si la
kibinadamu tu, kwa wale wanaosoma vitabu vitakatifu watakuwa na mifano
mingi ya watu waliowakosea wazazi wao wakalaaniwa.”
BABA DIAMOND ANASIKITISHA
Ijumaa lilipomtafuta
baba Diamond kwa njia ya simu aliongea maneno ya kusikitisha huku
akikataa katakata kumzungumzia kijana wake huyo.
“Jamani naomba mumuache Diamond na maisha yake, sitaki kabisa kusikia
habari zake maana hata nikiongea naonekana najipendekeza kwake.
“Namshukuru Mungu, kama ni kuumwa kwa sasa naendelea vizuri na maisha yangu, niacheni nipumzike,” alisema mzee huyo kwa unyonge.
DIAMOND ANASEMAJE?
Alipotafutwa Diamond ili
kumsikia anazungumziaje madai hayo, simu yake iliita bila kupokelewa.
Tunaamini atasoma habari hii hivyo si vibaya akatutafuta ili afunguke
kwa upande wake.
MAONI YA MHARIRI
Diamond ni staa mkubwa kwa sasa
ndani na nje ya Bongo, uwezo alionao kifedha unapaswa kuendana na
baraka za wazazi wa pande zote mbili. Vitabu vya Mungu vinatufundisha
kwamba wazazi ndiyo Miungu wetu hapa duniani hivyo hata kama kuna kosa
amefanya, mzazi atabaki kuwa mzazi tu. Hatutakiwi kumkosoa!