JESHI la Polisi Mkoa wa Kinondoni jijini Dar es Salaam linawashikilia 
watu watano wakiwamo askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa 
tuhuma za mauaji ya dereva wa Bajaj, Yohana Cyprian (20).
Watuhumiwa hao ambao majina yao hayakutajwa, wanadaiwa kumuua dereva 
huyo Aprili 3, mwaka huu, saa 9:00 mchana huko Mbezi Beach kwa Mboma 
jijini hapa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela aliwaeleza 
waandishi wa habari jana kuwa kuuawa kwa Cyprian kuliamsha hasira kwa 
baadhi ya wananchi.
Alisema kuwa wananchi hao walivamia Kituo cha Polisi Kawe kwa nia ya 
kumchukua mtuhumiwa aliyedaiwa kuwapeleka wanajeshi hao waliosababisha 
mauaji.
Kenyela aliongeza kuwa wananchi hao pia walizingira nyumba ya mmoja wa 
askari mgambo wakitaka kuichoma kwa lengo la kumuua na kulipiza kisasi.
“Baada ya kumuokoa mgambo huyo, wananchi walianza kuwarushia mawe na 
marungu askari kisha kuchoma matairi barabarani ili wamchukue mtuhumiwa 
na kumuua.
“Vurugu hizo zilidumu kwa saa mbili ndipo askari wakaamua kuwatawanya 
kwa mabomu ya machozi na risasi za baridi wananchi waliokuwa wanafanya 
vurugu,” alisema.
Kenyela aliwataja askari waliojeruhiwa kuwa ni E1739 D/CPL Alson, D.9054
 DCPL Felix na G.5407 PC Azizi aliyepigwa na jiwe kichwani.
Alifafanua kuwa katika vurugu hizo watu 12 walikamatwa na wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
chanzo;daima
 
 
 
 
 
 
No comments:
Post a Comment