MBUNGE WA MBARALI MKOANI MBEYA AHUKUMIWA KWENDA JELA MIEZI KUMI SOMA HAPA KOSA LAKE
MBUNGE wa Mbarali, Modestus Kilufi (CCM) amehukumiwa kifungo cha
miezi 10 baada ya kupatikana na hatia ya kutishia kuua, Mbunge huyo (51)
alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Oktoba 10 akidaiwa kutishia
kumuua Ofisa Mtendaji wa Kata ya Ruiwa, Mbarali, Jordan Masweve.
Kabla ya kusoma hukumu hiyo leo Mbunge aliomba Mahakama impunguzie
adhabu, kwani ana watoto watano kati yao wawili wanasoma Chuo Kikuu na
wananchi wanamtegemea kuwasilisha matatizo yao bungeni.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mbeya,
Michael Mteite, alisema ameridhika na ushahidi wa upande wa mashitaka
ukiongozwa na mawakili wa Serikali, Epimack Mabrouk na Griffin
Mwakapeje, pia mawakili wa upande wa mashitaka walimwomba Hakimu Mteite
kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa, ili iwe fundisho kwa watu wengine
wenye tabia kama hiyo.
"Kutokana na maelezo hayo na ushahidi ulioletwa mahakamani, ninakuhukumu kifungo cha miezi 10" alisema Hakimu Mteite.
Mbunge akihojiwa katika chumba cha mahakama alisema unajuwa siku
hizi haki inatendeka pale tu iwapo mwanaCCM ametiwa hatiani, lakini kama
ni mpinzani ametiwa hatiani utasikia ooh kaonewa au hii ni hukumu
kutoka ikulu, hata hivyo alisema atakata rufaa katika hukumu hiyo