Spika wa Bunge Anne Makinda juzi usiku alifunga mjadala
wa Bajeti Kuu ya Serikali, huku akiwaonya wabunge kwa kunukuu baadhi ya
vifungu vya Kanuni za Kudumu za Bunge inayoashiria kuwa ikiwa
hawatopitisha bajeti hiyo Rais atalivunja Bunge.
Akiahirisha kikao cha 53 cha Mkutano wa 11 wa
Bunge unaoendelea mjini Dodoma juzi usiku, Spika Makinda alitaja Kanuni
ya 107 (1) na (2) ambayo hutumika kukidhi matakwa ya Ibara ya 90 (2)(b)
ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayohusu Rais kulivunja
Bunge.
Kanuni hiyo ya 107.(1) inaeleza: “Mjadala kuhusu
Hotuba ya Bajeti ya Serikali utakapomalizika, Spika atalihoji Bunge ili
litoe uamuzi wake wa kupitisha au kutokupitisha Bajeti ya Serikali ili
kukidhi matakwa ya Ibara ya 90(2) (b) ya Katiba.”
Akinukuu kifungu hicho cha Katiba, Makinda
alisema: “Rais hawezi kulivunja Bunge, isipokuwa kama Bunge litakataa
kupitisha bajeti.”
Mjadala wa Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka
2013/14 umejadiliwa kwa siku nne kuanzia Jumatatu wiki hii ambapo
Makinda alisema kuwa wote walioomba kuchangia walifanya hivyo
wamekwisha.
“Nafunga mjadala wa Bajeti ya Serikali Kuu leo, wote walioomba na waliokuwepo wamekwisha,” alisema Spika Makinda.
Hata hivyo, wakichangia hotuba hiyo, wabunge wengi
walionyesha kupinga bajeti hiyo katika maeneo mbalimbali ikiwamo
misamaha ya kodi, ongezeko la kodi katika mafuta ya petrol na kodi ya
umiliki wa laini za simu (Simcard).
Wabunge pia walipinga bajeti hiyo wakitaka sekta
ya madini ichangie zaidi Pato la Taifa, kupitia na kurekebisha mikataba
ya madini.
Hali hiyo huenda inazua hofu kuwa huenda wabunge wengi wakaipinga kwa kuipigia kura ya hapana.
Kifungu cha 107(2) cha Kanuni za Kudumu za Bunge
inaelekeza kuwa uamuzi wa Bunge kupitisha au kutokupitisha Bajeti ya
Serikali utafanywa kwa kupiga kura ya wazi kwa kuita jina la mbunge
mmojammoja.
Jana Makinda alitangaza Jumatatu ijayo ya Juni 24
kuwa ndiyo siku ambapo wabunge watapiga kura kwa kuitwa majina
mmojammoja ili kupitisha Bajeti ya Serikali au la.
Hata hivyo, kurejea kwa wabunge wa Kambi Rasmi ya
Upinzani wa Chadema ambao hawakuchangia mjadala huo wa Bajeti Kuu ya
Serikali, hata kuwasilisha Bajeti Mbadala, kunaongeza hofu kuwa huenda
wabunge wote wa kambi hiyo wakaipinga.