"Hatua hiyo inachukuliwa dhidi yao kwakuwa sheria za Afrika Kusini zinatofautiana na sheria za Tanzania na ndiyo sababu hata Kamishna Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini, Geofrey Nzowa alikwenda nchini Afrika Kusini kufuatilia suala lao," kilisema chanzo hicho. Kwa upande wake Nzowa alipoulizwa alisema mzigo walioubeba Masogange na mwenzake haukuwa dawa za kulevya bali ni kemikali za dawa za kulevya.
Masongange
Hata hivyo Msemaji wa Mamlaka ya Mapato ya Afrika Kusini, (SARS), Marika Muller alieleza kuwa timu ya SARS ina uhakika kuwa mabegi sita yaliyokamatwa Julai 5 ni dawa za kulevya aina ya Methamphetamine. Wakati Masogange akitozwa faini hiyo mwenzake, Melissa Edward ameachiwa huru na mahakama hiyo, baada ya kukosekana ushahidi wa kumtia hatiani.
Msemaji wa Kitengo cha Uchunguzi wa Makosa ya Jinai cha Afrika Kusini(Hawk), Kapteni Paul Ramaloko akizungumza na Habarimpya.com mjini hapa jana alisema kwamba uchunguzi wa kisayansi uliomalizika jana umeonyesha kwamba watanzania hao hawakubeba dawa za kulevya, bali walibeba kemikali aina ephedrine ambazo pia hutumika kutengenezea dawa mbalimbali zikiwemo dawa za kulevya ambapo wakati mwingine hutumiwa na madaktari wakati wa upasuaji.
Kwa upande wa Melisa Kapteni Paul Ramaloko alisema kwamba Mahakama
ilibaini kuwa, hakuwa na kosa baada ya uchunguzi kuonyesha kuwa
alimsindikiza mwenzake katika safari hiyo na kwamba hakuhusika moja kwa
moja katika tukio hilo. “Mahakama iliona kuwa Melissa aliombwa tu
kumsaidia kubeba baadhi ya mabegi, lakini hayakuwa yake. Mizigo yote
iliandikwa jina la Agness Gerald na si Melissa,” alisema Kapteni
Ramaloko.
Mahakama Kuu ya Gauteng iliyoko eneo la Kempton Park jijini Johannesburg Afrika Kusini iliyokuwa ikiendesha kesi ya Masogange.
Kapteni Ramaloko alifafanua kwamba utetezi wa Melisa ulikubaliwa na Mahakama baada ya kujitetea kwamba walikutana na Agness ndani ya ndege na baada ya kuteremka, Masogange akamwomba amsaidie kubeba mizigo hiyo, kwani ilikuwa mikubwa. Kwa sheria za Afrika Kusini kubeba kemikali zozote ambazo zimepigwa marufuku ni kosa la jinai kisheria, hivyo mahakama iliamuru Masogange ahukumiwe kwenda jela kwa miezi 30 (miaka miwili na miezi mitano) au alipe faini ya R30, 000 (sawa na Sh4.8 milioni).
Hata hivyo, Kapteni Ramaloko alisema mdhamini wa Masogange alilipa nusu ya fedha na kwamba zinazobaki amalizie baadaye. Alisema
kutokana na kutomalizia kulipa fedha hizo ataendelea kubaki nchini humo
hadi atakapomaliza kulipa nusu ya faini iliyobaki. Masogange na mwenzake walipokamatwa na SARS ilielezwa walikuwa wamebeba dawa za kulevya aina ya Methamphetamine, lakini Mahakama juzi ilithibitisha walikamatwa na kemikali aina ya Ephedrine, ambayo siyo dawa za kulevya.