Kadri matatizo ya uzazi yanavyoendelea kukithiri duniani kote, wataalamu wa afya nao wanaendelea kuvumbua njia mbalimbali za kuwasaidia wenye matatizo ya kukosa watoto.
Katika harakati hizo Kliniki ya Upandikizaji ya
Dar es Salaam, (Dar IVF and fertility clinic) wameanzisha huduma ya
kununua mbegu za kiume na mayai ya wanawake, kwa ajili ya kutoa huduma
ya uzazi kwa njia ya upandikizaji au IVF.
Gazeti hili lilipiga simu katika kliniki hiyo
kutaka kujua iwapo linaweza kuchangia mayai na daktari aliyekuwapo zamu
alijibu; “inawezekana”.
Daktari huyo ambaye hata hivyo alisema kliniki
hiyo bado haijaruhusiwa kujitangaza katika vyombo vya habari, alisema
kwa sasa kifaa cha kuhifadhi mayai (ya mwanamke) hakipo ila kifaa cha
kuhifadhi mbegu za kiume kipo na wanapokea wachangiaji wanaotaka kuuza
mayai hayo kwa makubaliano rasmi.
“Ukija tutajadiliana bei, kwa sasa hatuna bei
rasmi, lakini nadhani ukija tutakubaliana. Siku ukiwa tayari njoo
tujadili. Bei ni makubaliano,” alisema daktari huyo.
Alisema kwa kuwa kifaa cha kuhifadhi mayai hakipo
hivyo mchangiaji atakapochangia mayai, yatatakiwa yatumike siku hiyo
hiyo katika upandikizaji, lakini kifaa cha kuhifadhi mbegu za kiume,
kipo.
Dk huyo (tunamuhifadhi jina kwa sababu ya sheria
za hospitali hiyo), alisema mchangiaji wa mbegu au mayai atatakiwa
kupimwa kwa kina, kwanza atapimwa damu kama ana maambukizi ya VVU,
atapimwa iwapo ana maradhi ya urithi na kundi la damu kabla ya
kukubaliwa kuchangia.
Tovuti ya kliniki hiyo inaeleza wazi huduma
zinazotolewa ambapo mbali na uchangiaji wa mbegu na mayai, lakini huduma
kuu ni kuwasaidia wenye matatizo ya uzazi, kupata watoto kwa njia ya
upandikizaji.
Huduma nyingine ni kutibu matatizo ya ugumba kwa
wanawake na wanaume, kuchagua jinsia ya mtoto, upasuaji wa kukaza kizazi
kuzuia mimba kutoka (shridkar shuture) pamoja na huduma za matenite.
Madhumuni ya watu kuchangia mbegu au mayai ni
katika kuhakikisha hakuna upungufu wa mbegu, na kuwasaidia wale wote
ambao wameshindwa kutimiza ndoto za kuwa na familia.
Dk Henry Mwakyoma, Daktari Bingwa wa masuala ya
uzazi wa Chuo Kikuu cha Tiba cha Muhimbili anasema, maendeleo hayo
yanafanikiwa zaidi nchi za nje ambako kuna teknolojia na utayari wa
watu.
“Kwa hapa kwetu kwanza teknolojia hii bado
haijapata umaarufu, lakini ni lazima kuhakikisha kuwa Watanzania wenyewe
wapo tayari kukubali uzazi wa njia hii,” alisema Dk Mwakyoma.