Waziri wa Katiba na Sheria, Mathis Chikawe amesema Rais Jakaya Kikwete hana mpango wa kuongeza muda wa uongozi wake baada ya 2015 kama baadhi ya wanasiasa wanavyodai.
Kadhalika, waziri huyo amesema hakuna sheria
inayomlazimisha Rais kusaini muswada wa sheria yoyote inayopitishwa na
Bunge na wala inayoweka muda maalumu wa kutekeleza wajibu huo.
Akizungumza na gazeti hili jana, Chikawe alisema
kwa vyovyote vile Rais Kikwete hawezi kuongeza muda wa kuwapo kwake
madarakani kwa kuwa anaheshimu Katiba ya nchi iliyomuweka madarakani.
Waziri huyo alitoa kauli hiyo baada ya kutakiwa na
gazeti hili kuzungumzia madai ambayo yamekuwa yakirudiwa mara kwa mara
na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba kwamba amenasa taarifa za
siri za kuwapo kwa mipango ya kuongeza muda wa Serikali ya sasa kukaa
madarakani.
“Ngoja nikwambie ndugu yangu, watu wanaongea tu,
kwanza Rais mwenyewe hana mpango huo, anasema kazi aliyonayo ni ngumu na
haoni sababu ya kuongeza muda,”alisema Chikawe na kuongeza:
“Mara zote ukizungumza naye anasema tuharakishe
mchakato wa Katiba na ikibidi tuingie katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 kama
Katiba yetu inavyosema kwa kuwa kazi aliyofanya inatosha kabisa.”
Mapema mwezi Mei mwaka huu, Profesa Lipumba
alisema kutokana na wasiwasi kwamba mchakato wa Katiba Mpya
hautakamilika 2014, hivyo Uchaguzi Mkuu hautaweza kufanyika.
Kuhusu hatima ya Uchaguzi Mkuu iwapo Katiba Mpya
itaanzisha mfumo wa Serikali tatu, Chikawe alisema: “Wananchi wasiwe na
wasiwasi ikifika wakati huo kila kitu tutajua, lazima tutakuwa na sheria
ya mpito ambayo itaweka mambo sawa mpaka kutufikisha katika Uchaguzi
Mkuu.”
Rais kusaini muswada
Chikawe pia alizungumzia hatima ya Marekebisho ya
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Mpya ambapo alisema hakuna sheria
inayomlazimisha Rais kusaini miswada inayopitishwa na Bunge.
“Hakuna sheria inayomlazimisha Rais asaini wala
kumpa muda wa kusaini, mwenyewe anatumia busara na hekima tu katika
kusaini sheria,”alisisitiza Chikawe.
Kauli ya Chikawe imekuja siku chache baada ya
wenyeviti wa vyama vya CUF, NCCR -Mageuzi na Chadema kutoa tamko la
kumtaka Rais Kikwete asisaini muswada huo mpaka pale yatakapokuwapo
maridhiano ya wadau muhimu kuhusu muswada huo. Alisema kwa kutokusaini
muswada huo, kunaweza kukaleta tafsiri mbili; kwanza ni wale wanaoweza
kutafsiri kuwa ni dharau kwa wabunge waliopitisha muswada huo, kwamba
walichofanya si sahihi na hakina maana.
CREDIT: MWANANCHI
CREDIT: MWANANCHI