BINTI wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Kilimani iliyopo
Kipunguni, Dar mwenye umri wa miaka 12 (jina tunalihifadhi kwa sababu za
kimaadili) amejikuta akishindwa kuendelea na masomo baada ya kupewa
ujauzito na kijana wa mtaani aliyejulikana kwa jina moja la Roja.
Akizungumza kwa huzuni mama wa mtoto huyo, Aziza Mohammed alisema
kuwa mwishoni mwa mwezi uliopita ndiyo aligundua kuwa binti yake huyo ni
mjamzito na ilikuwa ni baada ya kukataa kwenda shule huku akitapika
mara kwa mara.
Mama huyo alisema, baada ya kuona dalili hizo
aliamua kwenda kununua kifaa cha kupimia mimba lakini mwanaye huyo
alikimbilia kwa mama yake mdogo, Temeke ambako waligundua kuwa ni
mjamzito.
“Alipofika kwa mama yake mdogo ilibainika kuwa ana mimba,
wakanipa taarifa, nikawaomba wamlete kisha tukampeleka hospitali ambako
tulithibitishiwa na daktari kuwa kweli ana ujauzito wa miezi mitano,”
alisema mama huyo na kuongeza:
“Nilimbana aniambie mwenye mzigo huo
ambapo alimtaja kijana aitwaye Roja. Akaniambia kijana huyo ambaye ni
jirani yetu amekuwa akimbaka na kumtishia kumuua ikiwa atasema.
“Kwa
maelezo hayo ilibidi tumtaarifu mjumbe wa mtaa wa Kipunguni B, Bakari
Issa ambaye tulikwenda naye kutoa taarifa katika Kituo cha Polisi cha
Stakishari na kufungua jalada la kesi lenye namba STK/RB/18639/2013
KUMPA
MWANAFUNZI MIMBA
“Jamani naomba taasisi husika zinisaidie kwa
sababu baada ya kutoa ripoti polisi nimekuwa nikuzungushwa
tu...mtuhumiwa hakamatwi.”
SIMULIZI YA KUSIKITISHA
Binti aliyepata dhahama hiyo alipata
kuzungumza na Ijumaa ambapo alisimulia simulizi ya kusikitisha sana
ikionesha jinsi mchezo mzima ulivyokuwa.
Alisema: “Wadogo zake Roja
ndiyo walikuwa marafiki zangu...Roja alikuwa akiwatumia wao kuniita kila
siku jioni na nilipoenda alikuwa akinifungia chumbani kwake na
kunilazimisha kufanya naye mapenzi huku akinitishia kuwa nikisema
ataniua.
“Pamoja na vitisho hivyo alikuwa akinipa shilingi elfu tatu
hivyo nikawa naogopa kumwambia mama na nilipogundua nina mimba
nilimtuma wifi yangu (dada wa Roja) akamwambie lakini akakataa na kusema
mimba siyo ya ndugu yake, mimi sijawahi kufanya mapenzi na mwanaume
mwingine zaidi yake,” alisema binti huyo.
KUTOKA IJUMAA
Tukio hili linaumiza na kusikitisha. Ni wito wetu
kwa taasisi husika kufuatilia sakata hili na kumsaidia binti huyu ambaye
ndoto zake zimezimwa ghafla akiwa bado mdogo.
Aidha, ni vyema wazazi wakawa makini katika kufuatilia nyendo za watoto wao kabla mambo mabaya hayajawakuta.