Na Abu ‘ Ammaar
ALLAAN Subhaanahu Wata’ala
ametuneemesha na kutupa uhai tukaweza kufikia siku kumi bora kabisa katika
dunia ambazo Allaah Subhaanahu Wata’ala ameziapia katika Qur’aan, Suuratul
Fajr. Na Subhaana anapoliapia jambo lolote basi huwa lina umuhimu mkubwa na wa kipekee.
Neema hii ya kuwa tupo hai
na tuna afya njema ni jambo kubwa na muhimu sana kwa kila Muislamu kuzingatia.
Tayari tupo katika masiku
kumi bora katika mwezi wa Dhul Hijjah, kitu gani
tumenufaika nacho ndani ya masiku haya? Au siku hizi zinatupita tu kama siku
nyengine za kawaida?
Leo tunaingia tarehe 5 Dhul Hijjah
na kwa wengine ni 4 Dhul Hijjah Je tumeitumia fursa hii muhimu ya kukithirisha
kufanya Ibada ndani ya masiku haya?
Mtume Muhammad Swalla Allaahu ‘Alayhi
Wasallam anasema katika hadithi iliyopokelewa na Muslim kwamba: Hakuna siku ambayo Allaah (Subhaanahu Wata’ala) huwaachia waja (wake) huru na moto kama siku ya Arafah”
Allaah Subhaanahu Wat’ala katika
riwaya nyengine anasema kuwaaambia Malaaikah kwamba washuhudie jinsi Allaah
Subhaanahu Wata’ala alivyowasamehe waja wake. Mpaka Malaaikah katika kujaribu
kuhakikisha waliuliza ‘ Ee Allaah fulani amegubikwa na maasi na madhambi aina
kwa aina! Allaah Subhaanahu Wata’ala atawajibu, ‘Nimewasamehe wote’
Umuhimu wa siku ya Arafah unaweza
kueleweka vizuri kutokana na mazungumzo aliyobahatika kukabiliana nayo Amiirul
Muuminiyn ‘Umar bin Khattab, Allaah amuwie radhi, na myahudi mmoja aliekuwa
akiishi Madina wakati huo.
Siku moja Myahudi alikuja kwa ‘Umar
na kumwambia ‘Kuna aya katika kitabu chenu (cha Qur’aan) mnaisoma, lau kama aya
hii ingeliteremshwa kwetu Mayahudi basi siku ya kuteremshwa kwake ingelikuwa
siku kubwa sana kwetu ya kushereheka’ ‘Umar akamuuliza ni aya gani hiyo? Myahudi akamsomea
: ( الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ
لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمْ
الْإِسْلَامَ دِينًا) [ سورة المائدة:5
Leo
nimekukamilishieni dini yenu na kutimiza neema zangu kwenu na nimeridhia
UIslamu kuwa ndio Dini yenu. Al Maaidah 5
‘Umar akasema, 'bado naikumbuka
siku ambayo aya hii iliteremka ilikuwa ni siku ya Ijumaa na Mtume Swalla Allaahu
‘Alayhi Wasallam akihutubia tulipokuwa Arafah'
Naam myahudi
ameonesha thamani kubwa kuithamini siku bora kabisa katika siku za dunia, Je
mimi Muislamu na wewe ndugu yangu Muislamu unaesoma ujumbe huu umewahi kuipa thamani
inayostahiki siku ya Arafah ?.
Ni siku ambayo Dini yetu
ilikamilishwa, ni siku ambayo Allaah huwaachia huru na moto waja wake, ni siku
ambayo Allah Subhaanahu Wata’ala hutulipa thawabu za miaka miwili kwa kufunga
siku hii moja tu, ni siku ambayo tukiomba dua basi Allaah atatukabalia dua zetu,
ni siku ambayo Shetani anaichukia anapoona Rehma za Allaah Subhaanahu Wata’ala zinavyomwagwa
kwa waja na hujawa na tahayari na ghera
mpaka kufikia kujitia mchanga usoni kwa soni na tahayari kama alivyosimulia
Mtume Swalla Allaahu ‘Alayhi Wasallam katika hadithi iliyopokelewa na Ahmad.
Ndugu yangu katika imani, tuwe
pamoja katika kufanya mambo ya kheri katika masiku kumi ya kheri na tuhakikishe
tunatia Nia ya kufunga siku ya Arafah.
Tuwakumbushe na wengine umuhimu
wa kuifunga siku hii na tumuombe Subhaana atawafikishe tuifikie siku hii adhimu
katika hali ya afya na siha na kutuwezesha kufunga kwa ajili ya kupata radhi
zake Subhaana.
Aamiyn Aamiyn
Aamiyn Aamiyn