"SITASAHAU MWANANGU ALIPOMFUATA MAREHEMU SAYUKI".....VANITHA
Leo tunaye muigizaji mkongwe aliyeanza kuwika kupitia Tamthiliya ya Jumba la Dhahabu miaka ya zamani, Vanitha Omary.
Msanii huyu ambaye ameonesha cheche zake kwenye filamu za Viola, Between, Five Question, Ukungu na nyingine kibao, ana watoto wawili, Precious (3) na Paulsen (6) ambao anaishi nao pamoja na mume wake (Mtenda) maeneo ya Mwananyamala, jijini Dar.
Ili kumjua zaidi, ungana nami katika mahojiano ambayo nimefanya naye:
Mdadisi Mambo: Leo nimekutembelea kwako, vipi wazima lakini?
Vanitha: Sisi hatujambo, enhe nambie bila shaka una jambo, si bure.
Mdadisi Mambo: Hapana, nataka kujua maisha yako na wanao pindi mnapokuwa nyumbani.
Vanitha: Oke, maisha ya mimi na wanangu ni mazuri sana.
Mdadisi Mambo: Uzuri wake upoje?
Vanitha: Ninapokuwa na wanangu huwa sikasiriki yaani hata nikiudhiwa kazini, ninapoingia ndani najikuta nikitabasamu.
Mdadisi Mambo: Najua uko bize sana na sanaa, unapata muda kweli wa kuwalea wanao?
Vanitha: Ni kujipanga tu, hakuna kinachoharibika kwani watoto wangu wanapata malezi kama kawaida.
Mdadisi Mambo: Ni kitu gani ambacho watoto wako waliwahi kukifanya huwezi kukisahau?
Vanitha: Ni siku mwanangu mkubwa (Paulsen) alipopotea halafu akasema alikwenda kwa marehemu Sajuki ambaye kipindi hicho alikuwa na mwezi mmoja tangu afariki.
Mdadisi Mambo: Duu hiyo kali, ikawaje sasa?
Vanitha: Baada ya kumpeleleza kwa muda mrefu, hakubadilisha kauli yake, alisisitiza kuwa alikwenda kwa Sajuki, sitokaa nikisahau kisa hicho.
Mdadisi Mambo: Nini ambacho hukipendi kitokee kwa wanao?
Vanitha: Sipendi mtu yeyote amnyanyase mwanangu au kusema baya juu yao, ataniudhi.
Mdadisi Mambo: hivi huwa unawachapa wanao pindi wanapokosea?
Vanitha: Wanapofanya kosa lazima wapate adhabu, mimi ni marafiki zangu lakini wanapokosea lazima niwakanye.
Mdadisi Mambo: Ni kitu gani ambacho hukipendi kitokee katika maisha ya wanao?
Vanitha: Sipendi wafanyiwe vitendo vya udhalilishwaji wa kijinsia au vitendo vyoyote vya kikatili.
Mdadisi Mambo: Haya Vanitha, nashukuru sana.
Vanitha: Nashukuru na mimi, karibu tena.