JESHI
la polisi nchini limefanikiwa kuisambaratisha ndoa ya mwanafunzi wa
kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Mboga iliyopo Chalinze
mkoani Pwani, Asha Daru mwenye umri wa miaka 15, aliyeozeshwa kwa Said
Ally (29), mkazi wa Pugu jijini Dar, Ijumaa iliyopita.
Ndoa hiyo
iliyotawaliwa na usiri mkubwa, ilifungwa nyumbani kwa bibi wa mwanafunzi
huyo aitwaye Asha Abdallah maeneo ya Tandale Kwamtogole, Dar.
Kuvuja
kwa siri ya ndoa hiyo kulifanikishwa na mmoja wa ndugu wa familia ya
mwanafunzi huyo ambaye alidai kitendo hicho kilimkera hivyo kuwaomba
mapaparazi wa Oparesheni Fichua Maovu (OFM)kumnusuru binti huyo mdogo aliyedaiwa kulazimishwa kuolewa.
Baada
ya kumsikiliza kwa umakini ndugu huyo mwenye mvi za hekima, mapaparazi
wetu walilishirikisha jeshi la polisi na kuanza kuwafanyia mtego wa
kuwanasa waliokuwa wakifanikisha tukio hilo.
BWANA HARUSI AWASILI UKWENI
Mishale ya saa 4:00 asubuhi kama
ilivyoripotiwa na mtoa habari wetu, tayari bwana harusi ambaye ni fundi
seremala alikuwa akiwasili ukweni na kupokelewa na nderemo za chinichini
huku mapaparazi wetu wakiwa wamezingira eneo hilo.
Mapaparazi wetu
walifanya upekepeke na kuingia hadi chumba cha bi harusi mtarajiwa na
kumkuta shangazi yake akimpamba fastafasta kwa kile ilichoonekana kama
walichelewa kumaliza kazi hiyo hadi ndoa inaanza kufungwa.
USTAADHI AMWAGA MAWAIDHA NA NDOA
Makachero wa jeshi la polisi na
OFM, wakiwa kama wageni waalikwa, walisubiri kila kitu kiendelee ili
kupata ushahidi wa tukio ambapo ustaadhi aliyekuwa akifungisha ndoa hiyo
alionekana akimfungisha Said ambaye alitamka mbele ya waozaji na wageni
wengine wakiwemo makachero kuwa anamuoa binti huyo kwa mahari ya
shilingi laki tatu na nusu ambapo alilipa laki mbili na kubakiza deni la
laki moja na nusu.
Baada ya tamko hilo, zilisikika nderemo za chinichini kutoka chumbani kwa bi harusi.
Huku
nderemo zikiendelea, ustaadhi aliyekuwa akifungisha ndoa hiyo alianza
kutoa mawaidha ya ndoa akiwausia maharusi kuishi kwa maadili ya
kumpendeza Mungu na kuijaza dunia kama watajaliwa.
POLISI WAVAMIA
KATIKATI YA SHEREHE
Mambo
yakiwa yamenoga huku polisi wakisubiri wahusika wamalize mambo yao,
inspekta wa jeshi la polisi aliyevalia kiraia akiwa na ‘mkwaju kiunoni’
alisimama na kujitambulisha kwa jina la Inspekta Rodger na kuwaweka
chini ya ulinzi bwana harusi, ustaadhi, bi harusi, bibi yake na ndugu
wengine waliokuwa eneo hilo.
Wote wakiwa chini ya ulinzi, Inspekta
Rodger aliwatajia tuhuma zao na kuwaita vijana wake waliotanda eneo hilo
na kuwaamuru kuwakamata watuhumiwa wote na kuwatia kwenye ‘difenda’
msobemsobe kwa ajili ya safari ya kuelekea Kituo cha Polisi cha
Magomeni, Dar kutoa maelezo.
MAHARUSI WATIWA KWENYE DIFENDA
Maharusi waliongozwa na kupandishwa
kwenye difenda na kufuatiwa na ustaadhi, bibi wa bi harusi, mshenga
aliyefahamika kwa jina la mama Batenga na ndugu wengine.
BIBI AMWAGA TAMBO KITUONI
Wakiwa kituo cha polisi, bibi wa bi
harusi alikuwa akijigamba kuwa ndoa hiyo ya mjukuu wake ni halali na
kusema umri wa miaka 15 alionao siyo sababu ya kukosa kuolewa.
Akimzungumzia binti huyo mwanafunzi, bibi huyo alisema aliamua kumuoza
mjukuu wake huyo kwa kuwa alikuwa hapendi shule na alikuwa amekubuhu kwa
utoro hivyo akaona ni bora aende kwa mume.
“Kwani mtu kuolewa na
miaka 15 ni ajabu gani? Sisi Waluguru kwetu tunaolewa hata chini ya
miaka hiyo, mimi mwenyewe huyu babu yake amenioa nikiwa na miaka 15,
sasa leo ajabu iko wapi?” alihoji bibi huyo.
BWANA HARUSI ALALA LUPANGO
Ulipofikia wakati wa kutoa maelezo,
bwana harusi alisema kwamba yeye aliambiwa mkewe mtarajiwa alikuwa na
umri wa miaka 18 na angejua kama ana umri huo asingemuoa.
Licha ya
utetezi huo, sheria iliendelea kumbana kwa kufanya kosa hilo ambapo
alifunguliwa kesi ya jaribio la ubakaji kisha akaswekwa lupango.
Wengine
waliowekwa rumande kwenye tukio hilo ni baba wa bi harusi, Daru
Abdallah, bibi wa bi harusi, Asha Abdallah, mjomba wa bi harusi ambaye
jina lake halikuweza kupatikana pamoja na mshenga.
Bi harusi huyo yeye alipelekwa ustawi wa jamii kwa ajili ya mchakato wa kuangalia mustakabali wa maisha yake.